Simulizi :
Mtikisiko Wa Hirizi
Sehemu Ya Pili (2)
Kwa hesabu ya
muuzaji, hata kama angeuza mavazi hayo kwa shilingi 12,000 bado angekuwa na
faida. Isitoshe, hakuwa ameuza hata nguo moja katika nguo hizo tangu alipozileta
kiasi cha mwezi mmoja uliopita. Hivyo, hakuwa na sababu ya
kukataa.
“Leta pesa.”
Muda mfupi baadaye Shaka
alikuwa katika mwonekano tofauti. Alitumia chini ya dakika mbili kuvaa zile nguo
za uraiani juu ya mavazi ya jela huku yule muuzaji akiwa amepigwa
butwaa.
Bado Shaka hakuwa amehitimisha kilichomleta humo.
Akaendelea kuangaza huku na kule. Macho yakagota sehemu ambayo kulitundikwa visu
vya aina mbalimbali na vya ukubwa uliotofautiana.
“Kile kisu
bei gani?”
“Alfu mbili na mia
tano.”
“Nipe.”
Kisu kikatua mfukoni mwake.
Akatoka hapo kwa mwendo wake uleule, mwendo wa taratibu na wa kujiamini. Na sasa
hakutaka kuchelewa katika eneo hilo, alikodi teksi iliyomfikisha Magomeni Kondoa
ambako alipata chumba katika gesti moja isiyokuwa na
hadhi.
Mara tu alipokwishaingia chumbani na kujifungia,
alizivua zile sare za jela na kuzifutika chini ya kitanda. Akabaki na zile nguo
mpya pekee. Kisha akatoka na kwenda dukani ambako alinunua lita moja ya mafuta
ya taa na kurejea pale gesti.
“Nionyeshe sehemu ya kuweza
kuchomea makabrasha nisiyoyahitaji,” alimwambia mhudumu wa
gesti.
Mhudumu huyo, akiwa hajui hili wala lile, alimwonesha
sehemu kulikokuwa na shimo dogo lililotumika kwa kutupia taka. Shaka aliporudi
chumbani alizitwaa zile nguo za jela, zilizokuwa ndani ya fuko la nailoni,
akatokanazo hadi huko shimoni ambako alizimwagia mafuta na kuzitia
moto.
Alirudi chumbani mwake baada ya kuhakikisha kuwa zile
nguo zote za jela zimeteketea.
*******
ASKARI
jela aliyesimamia kundi la wafungwa waliopaswa kwenda Viwanja vya Maonesho,
aliendelea kuduwaa huku akimtazama Shaka aliyekuwa akiyoyoma taratibu machoni
pake. Huenda alipaswa kuchukua hatua pale tu Shaka alipokaidi amri ya kuingia
garini, lakini hakufanya hivyo. Na alipokuja kuzinduka, Shaka alikuwa
ameshatokomea machoni pake.
Akakurupuka kupuliza filimbi. Eneo
hilo lote likazingirwa na askari, na wengine wakamwagwa mitaani kumsaka mfungwa
aliyetoroka katika mazingira ya kutatanisha.
Pamoja na msaada
wa raia wema waliowaonesha njia alizopita mtu aliyekuwa amevaa nguo
zilizoshabihiana kwa kila kitu na sare za wafungwa wa jela, na pamoja na
mwanamke muuza duka kuthibitisha kufikiwa na mteja aliyevaa sare za jela na
kuongeza kuwa mteja huyo alinunua nguo mpya na kuzivalia humohumo dukani, juu ya
mavazi ya jela, bado haukuwa msaada ulioweza kutoa matunda mema.
Shaka hakuonekana, japo
msako mkali uliendelea takriban kitongoji chote cha Keko.
Naam,
kilikuwa ni kizungumkuti cha aina
yake!
********
AKITAMBUA fika kuwa lazima
msako mkali dhidi yake ungefanyika, Shaka hakutoka nje ya gesti hiyo siku nzima.
Njaa ilipomsakama alimtuma chipsi mhudumu wa gesti. Koo lilipomkauka aliagiza
bia. Kwa jumla alihakikisha hafanyi kosa atakalolijutia baadaye. Japo aliamini
kuwa kwa ‘nguvu’ za baba yake, Mzee Songoro, asingepatwa na baya lolote, hata
hivyo aliamua kuwa makini.
Usiku ulipoingia alihitaji faraja ya
mwanamke. Ndiyo, usiku kucha awe na mwanamke mrembo, mwanamke anayeyajua
majukumu yake pale anapokumbana na mwanamume mwenye njaa ya
mwanamke.
Bia tano zilizosambaa katika mishipa yake ya damu
zilimpa mhemuko kiasi cha kuamua kuzungumza kiutu uzima na mhudumu mmoja wa kike
wa gesti hiyo, mazungumzo yaliyoanzia kwa ‘gia’ ndogo tu, bia mbili, chipsi-kuku
na shilingi 10,000.
Usiku huo ukawa wao. Wakakesha wakizungumza
kwa furaha, wakanywa kwa kujidai na wakaikanda miili yao kwa fahari, wakifanya
kila walichopenda kukifanya, na wakafanya kwa namna ya kipekee kiasi cha
kujikuta kukipambazuka huku kila mmoja bado akimhitaji
mwenzie.
Hata hivyo, Shaka hakuwa limbukeni wa mapenzi. Kwa
siku hii, zikiwa ni saa zisizozidi ishirini na nne tangu alipotoroka gerezani,
aliamua kuwa makini zaidi na kuzitumia fedha zake chache alizonazo kwa uangalifu
ili awe na uhakika wa kuliacha jiji hilo na aweze kufika mwisho wa safari
yake.
Akiwa bado kitandani, mkono wake mmoja ukilipapasa paja
la Rukia, alikuwa akiwaza hili na lile kuhusu ratiba yake ya siku hiyo huku pia
akifikiria ni hatua gani ambayo askari watakuwa wameichukua baada ya kutoroka
gerezani jana katika mazingira ya kutatanisha.
Aliamini kuwa
kwa vyovyote vile nguvu ya msako dhidi yake itakuwa kubwa na ikiambatana na
hasira kali kutoka kwa hao askari. Kwa kiasi fulani itachukuliwa kuwa
amelidhalilisha Jeshi la Magereza.
Itakuwa ni habari kubwa kwa
vyombo mbalimbali vya habari hususan vile vyenye sera ya kuishambulia serikali
kwa dosari yoyote itakayojitokeza katika taasisi zake. Itakuwa ni kashfa kwa
Jeshi la Magereza. Kwa hali hiyo alipaswa kuwa makini zaidi katika muda
atakaokuwa jijini Dar es Salaam.
Alipaswa kuchukua tahadhari
kubwa!
Ni Rukia aliyemwingilia katika fikra zake. “Vipi,
mpenzi, na jioni tutakuwa wote?” alimuuliza.
“Nd’o maana’ake,”
Shaka alijibu huku akitambua fika kuwa alikuwa akiongopa. Kumchukua mwanamke
huyo jana usiku siyo kwamba alikuwa na chembechembe za mapenzi kwake. Hapana.
Kwa kipindi hicho hakuwa ni mtu wa kumpenda wala kumwamini mwanamke yeyote. Ni
tamaa ya kimwili tu iliyomwangusha kwa Rukia.
“Tutakuwa wote,”
aliongeza huku akiendelea kulipapasa paja lake. “Umeonyesha kuwa ni mwanamke wa
shoka. Kwa vyovyote vile bwana’ko anaringa na kujisikia fahari kuwa na
wewe.”
“Nani kakwambia kuwa nina bwana?” Rukia aliuliza huku
akijitia kukasirika, akaukunja uso na kumtazama Shaka kwa macho
makali.
“Mwanamke mzuri kiasi
hiki, mwenye sura inayovutia na umbo linalotamanisha, mwanamke unayejua kumtoa
jasho mwanamume mwenye uchu wa ngono, uwe huna bwana?” Shaka alitiririsha maneno
bila ya kutishwa na macho yale.
Rukia alicheka kidogo kisha
akasema, “Amini usiamini, mie niko peke yangu. Sina mume wala sina hawara hapa
Dar.”
“Kwa nini?”
“Basi tu, nimeamua. Ni wewe
nd’o nimejikuta nakuvulia nguo tangu niachane na aliyekuwa bwana’ngu kiasi cha
miaka mitano iliyopita.”
Shaka hakuwa mtu wa kumwamini mwanamke
mapema kiasi hicho. Hata hivyo hakutaka kuuendeleza mjadala huo. Badala yake
akasema, “Ok, nimekuelewa mrembo. Sidhani kama utakuwa umenihadaa. Nakuamini. Ni
kwa kuwa tu muda huu nina majukumu mengine lakini kama siyo hivyo, nilitaka
tuendelee kujichimbia hadi jioni.”
“Na
njaa?”
“Yap, na njaa yetu.”
Rukia alicheka
kidogo. Akaupeleka mkono wake mahala fulani mwilini mwa Shaka ambako ulifinya
kidogo kiasi cha Shaka kujikuta akipumua kwa nguvu, mwili
ukimsisimka.
“Kwa hiyo itakuwaje?” Rukia
aliuliza.
“Saa mbili usiku tuonane,” Shaka alijibu. “Wewe si
upo hapahapa?”
“Hapana. Nina kwangu. Hapa ni kazini tu. Saa
hizi nitatoka, nitarudi saa nane mchana.”
“Poa. Kwa hiyo ni
kama nilivyokwambia. Mi’ nitakuwa humu ndani kuanzia saa mbili
usiku.”
*****
RUKIA alipoondoka, Shaka aliingia bafuni
haraka, akaoga kisha akamfuata kijana mmoja wa kiume ambaye ndiye aliyekuwa
mhudumu wa mapokezi asubuhi hiyo. Akampatia shilingi 7,000 huku akimwambia,
“Niletee magazeti yote ya leo.”
“Yote ya leo?” kijana yule
alishangaa. “Mbona kila siku yanatoka magazeti mengi sana! Pesa hii
itatosha?”
“Magazeti ya kila siku!” Shaka alisisitiza. “ Siyo
gazeti linalotoka leo na kutoka tena baada ya siku tatu au wiki. Nataka magazeti
yanayotoka tangu Jumatatu hadi Jumapili. Umenielewa?”
“Ya
Kiingereza na Kiswahili?”
“Ya Kiswahili
tu!”
“Nimekusoma mkuu.”
Kijana huyo alitoka na
kurejea baada ya dakika kumi, mkononi akiwa na magazeti saba ya Kiswahili. Mara
tu alipokwishamkabidhi Shaka magazeti hayo, alitoka huku akimwangalia kwa namna
ya kumshangaa.
Shaka hakumjali, alijilaza kitandani na kuanza
kuyapitia magazeti hayo. Magazeti yote yalikuwa na tangazo lililohusu kutoroka
kwake gerezani, tangazo lililoambatana na picha yake kubwa katika ukurasa wa
mbele!
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
TANGAZO hilo
lilinakshiwa na ahadi ya zawadi nono ya shilingi milioni kumi kwa yeyote
atakayefanikisha kukamatwa kwake.
Alitarajia kuwa tangazo hilo
lingetolewa kwenye vyombo mbalimbali vya habari yakiwamo magazeti, redio na
televisheni na picha yake kutumika katika kuikoleza habari au tangazo hilo.
Lakini hakutarajia kuwa magazeti yote yatokayo kila siku kwa lugha ya Kiswahili
yangetoa tangazo hilo. Alidhani kuwa gazeti moja au mawili tu ndiyo yangetumika
na tangazo hilo au habari hiyo ingekuwa katika kurasa za ndani, siyo
mbele!
Hali hii ilimtia shaka na akahisi kuwa kuendelea
kujichimbia hapo gesti hata kwa nusu siku kusingemsaidia, zaidi kungempeleka
katika matatizo.
Akayatupa magazeti yote kitandani. Akasimama
na kuzichomoa fedha zilizokuwa mfukoni mwake. Akaguna. Zilikuwa ni shilingi
50,000 tu. Hakushangaa, aliyakumbuka matumizi ya jana yake; nguo, kisu, teksi,
chakula, bia, gharama ya chumba na zile 10,000/- alizompatia Rukia kwa
makubaliano ya kumstarehesha usiku.
Hizi fedha alizonazo si
lolote si chochote kama atataka kwenda Kigoma. Zisingeweza kumfikisha popote.
Ili aweze kufika huko kwa kutumia usafiri wa treni alipaswa kutumia si chini ya
shilingi 50,000 kwa usafiri wa daraja la tatu, na hapo bado akiwa na upungufu wa
fedha za matumizi njiani mathalani kula na kadhalika.
Kama
atataka kutumia usafiri wa basi, itabidi ajipinde upya kusaka nyongeza.
Zingehitajika si chini ya shilingi 70,000! Kwa upande wa treni, aliona kuna
kizungumkuti cha aina yake. Aliuona usafiri huo kama haustahili kuendelea
kuwepo. Tangu Shirika la Reli libinafsishwe, utaratibu wa usafiri umekuwa
haueleweki. Mara leo treni ipo, mara haipo, mara leo treni ya mizigo imepinduka
na kuziba njia, matokeo yake zinapita siku sita hata wiki kwa ukarabati, usafiri
hakuna!
Hadi asubuhi hii hakuwa na taarifa yoyote kuhusu
usafiri wa treni kwa siku hiyo. Na hakuwa na muda wa kufuatilia. Muhimu kwake
ilikuwa ni kupata pesa zaidi na kuiacha Dar, basi! Kama ataondoka kwa treni,
Ndege, lori au basi, hilo litajulikana mbele kwa mbele.
Wazo
moja likamjia akilini. Ubabe. Atumie ubabe ili aongeze kipato na kwa kutumia
ubabe huohuo apate usafiri wa kumfikisha Morogoro au hata Dodoma ambako
angetumia mbinu nyingine kupata usafiri wa kumfikisha
Kigoma.
Mara akatoka chumbani humo kwa hatua ndefu hadi
mapokezi. Hapo akasita baada ya kutomkuta mhudumu. Hakujali, zaidi alifurahi kwa
kutomkuta kwani hakuwa na muda zaidi wa kuzungumza naye, isitoshe alishakuwa na
shaka kuwa huenda akawa amezitazama vizuri picha zilizotanda kwenye magazeti
yale manne ya Kiswahili na hivyo kuamua kwenda kuripoti kituo cha
Polisi.
Hakuendelea kuduwaa eneo hilo. Alitoka na kuingia
mitaani. Baada ya kuvuka mitaa miwili, mitatu mara akasimama kwenye duka moja.
Hapo akanunua kofia pana na kutoka baada ya kukosa miwani. Akaendelea kukata
mitaa.
Hatimaye akakutana na kijana mmoja, maarufu kwa jina la
‘Machinga’ akiuza miwani. Akanunua moja na kuipachika usoni papohapo. Naam, sasa
akajiona yu timamu, na tayari kwa safari!
Ni eneo hilohilo la
Magomeni, kando ya kituo cha daladala cha Usalama ndipo alipotarajia kupatumia
kwa kuianzia safari yake. Kutoka hapo aliponunua miwani hadi kwenye kituo hicho
kulikuwa ni umbali wa hatua kama mia moja au mia mbili hivi. Akavuta hatua ndefu
akielekea mahali hapo.
Mara akaamua kuvuka barabara hiyo na kushuka
upande wa pili ambako kuna baa mbili ambazo kwa wakati huo kulikuwa na watu
wachache walioketi chini ya miti baadhi wakinywa soda, baadhi wakinywa bia na
baadhi wakiwa wamekaa tu labda kwa kufuata kivuli.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mbele kidogo kulikuwa
na teksi zisizopungua kumi kituoni hapo, baadhi zikiwa na utambulisho rasmi kuwa
ni teksi halali, na nyingine zikiwa ni zile ambazo huitwa ‘teksi
bubu.’
Yeye hakujali uhalali au uharamu wa teksi, alijali
ubora.
Mbele yake aliiona teksi moja maridadi, akaifuata. Alipoifikia na
kuchungulia ndani akamwona dereva kaegemea kiti, usingizi umemteka. Akamgusa
bega kidogo. Dereva akashtuka na kufikicha macho. Akajiweka vizuri kitini.
Kisha: “Karibu anko, karibu sana.”
Shaka hakujibu, alifungua
mlango wa mbele, kushoto na kujipweteka kitini. “N’ambie, gari iko
fiti?”
“Iko fiti, mjomba,” dereva alijibu. “Hapa nd’o umekuta
gari. Hiki ni chuma cha reli.”
“Mafuta? Tukiondoka hapa, sio
unasema eti unapitia petrol station.”
“Hapana,” dereva alijibu
haraka. “Mimi sio kama madereva teksi wengine. Nina mafuta ya
kutosha.”
“Kiasi gani?”
Dereva alifikiri
kidogo kisha akajibu, “Kama lita kumi, hivi.”
“Ok, twende.
Shika Morogoro Road. Tukifika Ubungo nitakuelekeza
zaidi.”
Teksi iliondoka taratibu katika eneo hilo. Walipofika
Ubungo dereva akasema, “Tuko Ubungo, mzee.
Inakuwaje?”
“Twende!”
Gari likazidi kusaga
lami. Wakafika Kimara.
Wakaivuka.
“Tunakwenda
mbali, mzee?” hatimaye tena dereva alihoji.
Kwa kiasi fulani
alianza kuingiwa na wasiwasi. Hakutarajia kuwa wangekuwa na safari ndefu kiasi
hicho. Kama angejua, angewahi kutamka kiwango cha nauli iliyopaswa kulipwa.
Sasa walikuwa wakiipita Mbezi.
“Ni Kibamba. Kama
tatizo lako ni pesa, nipe chaji yako.”
“Kwenda na
kurudi?”
“Kwenda tu.”
“Hamsini tu, mzee
wangu.”
“Nakupa
arobaini.”
“Poa.”
**********
TEMBA,
kijana aliyetumwa na Shaka kununua magazeti, alijawa na dukuduku kila
alipozitazama picha za kurasa za mbele za baadhi ya magazeti hayo. Akiwa ndiye
aliyewapokea wageni wote wa gesti hiyo siku iliyopita, tayari alikwishaikariri
vizuri sura ya Shaka.
Alichokifanya mara tu baada ya kumkabidhi
Shaka magazeti yake ni kwenda kununua gazeti lingine moja. Na hakurudi kule
gesti moja kwa moja bali aliganda sehemu fulani na kulisoma kwa kina tangazo
lile sanjari na kuitazama kwa makini zaidi picha husika iliyokuwa na maelezo
chini yake:
JINA: SHAKA SONGORO
KABILA:
MMANYEMA
DINI: HAIJULIKANI
UMRI: MIAKA
35-40
MWENYE PICHA HIYO HAPO JUU NI JAMBAZI HATARI ALIYEKUWA
AKITUMIKIA KIFUNGO KATIKA GEREZA LA KEKO JIJINI DAR ES SALAAM. KATIKA MAZINGIRA
YA KUTATANISHA MTU HUYO AMETOROKA AKIWA CHINI YA ULINZI. ZAWADI NONO YA SHILINGI
MILIONI KUMI (10,000,000/-) ITATOLEWA KWA YEYOTE ATAKAYEFANIKISHA UPATIKANAJI
WAKE.
Temba akashusha pumzi ndefu na kuanza tena kutembea
akielekea gesti. Alipofika aliingia moja kwa moja kwenye chumba kilichotumiwa
kwa kuhifadhi shuka na vifaa vingine vya gesti hiyo. Huko alimkuta Mado, mmoja
wa wafanyakazi wenzake akiwa anafanya usafi.
“Mado,” alimwita
kwa sauti ya mnong’ono huku akiingia chumbani humo na kuurudishia mlango. Akampa
gazeti lile huku akimwonyesha picha ile iliyoutawala ukurasa wa
mbele.
Mado aliitazama picha ile kwa makini kisha akasema, “Hii sura
siyo ngeni sana machoni mwangu.”
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unadhani umeshamwona
wapi?”
“Sikumbuki. Lakini kama sio jana basi juzi nimemtia
machoni.”
Temba akacheka kidogo kisha akasema, “Soma maelezo hayo hapo
chini.”
Mado alitulia na kuyasoma maelezo kwa makini. Hatimaye
akahema kwa nguvu na kunong’ona, “Anaitwa Shaka Songoro.”
“Na
kuna bonge la mshiko kwa atakayemtosa kwa maafande,” Temba alidakia. “Milioni
kumi ziko nje, nje mwanangu!”
“Upuuzi,” Mado aliponda. “Dar ni
kubwa sana. Isitoshe jamaa mwenyewe huyo sio bwege, mwanangu. Hawezi kuwa bado
anabunya-bunya na kumbwela-mbwela kwenye mitaa hii ya Dar. Mtu anajua fika kuwa
atasakwa, sa’ unafikiri atalemaa hivihivi? Atakuwa kishasepa
mwana.”
Ukimya wa kitambo kifupi ulitawala, Mado na Temba
wakitazamana. Kisha Mado akasema, “Achana na dili hilo lisilokuwa na
maana…”
“Hapana, Mado,” Temba alimkata kauli. “Nina wasiwasi na
mtu mmoja.”
“Nani?”
“Huyu jamaa aliyeingia
jana.”
“Yule bonge la mtu?”
“Ndiyo. Hebu
itazame vizuri picha hii.”
Kwa mara nyingine Mado aliikazia
macho picha ile kisha akaguna. Akaunyanyua uso na kumkazia macho
Temba.
“Kwani huyu jamaa anaitwa nani?”
“Sijui
anaitwa nani. Tatizo hapa tunafanya biashara kisirisiri.
Hakuna
cha leseni na wala hatulipii kodi ya mapato. Mteja akija ni kuongea naye tu na
kupeana malipo, basi. Haandikishwi kwenye leja wala
nini.”
“Tabia yake umeionaje?”
“Ni hiyo
inayonishangaza,” Temba alijibu. “Aliingia jana kitu kama saa nne hivi, asubuhi.
Na hakutoka tena. Msosi aliagiza, bia pia aliagiza. Usiku kucha akawa na
Rukia.”
“Anaweza kuwa ni yeye?!”
“Kwa asilimia
tisini na tano naamini ni yeye!” Temba alisema kwa
msisitizo.
“Na hadi muda huu yuko
chumbani?”
“Atakuwemo! Nimempelekea magazeti yake muda huuhuu,
kama dakika kumi zilizopita.”
“Basi kumbe shwari tu,” Mado
alisema huku akiacha kila alichokuwa akikifanya. Akaongeza, “Kuna milioni kumi
za bure! Zinaelea-elea tu kudadadadadadeeeeek! Hakuna
kuziacha!”
Wakati wakikurupuka kutoka chumbani humo, hawakuwa
wakijua Shaka alikuwa akiwaza nini chumbani alikokuwa.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
********
“PAKI
pembeni, kuna dharura,” Shaka alimwamuru dereva teksi. Wakati huo walikuwa
katika eneo lisilokuwa na watu wala nyumba yoyote.
Dereva
alitii amri hiyo.
Mara Shaka akaangaza macho huku na kule;
mbele, nyuma, kushoto na kulia kisha akakichomoa kisu chake taratibu bila ya
dereva yule kugundua.
Kwa wepesi wa aina yake, akitumia
asilimia kubwa ya nguvu alizojaaliwa, alikitumbukiza kisu kile tumboni mwa
dereva kisha akakichomoa na kukizamisha mara mbili kifuani! Damu nyingi ilimtoka
dereva yule, na Shaka alikuwa makini kuhakikisha kuwa damu hiyo haimrukii.
Akimwinamisha huku kamziba kinywa ili asipige kelele.
Alimwacha
katika hali hiyo hadi alipohakikisha kuwa amekata roho. Kilichofuata ni kumpekua
mifukoni ambako alikuta fedha, shilingi 50,000. Akazichukua na kuzitia katika
himaya yake.
Hakuwa tayari kuendelea kuwa na maiti hiyo humo
garini, hivyo alipogundua kuwa hakukuwa na mtu yeyote ambaye angemwona, na wala
hakukuwa na gari lolote lililokuwa likija, alimtoa garini, akamburuta hadi kando
ya barabara, nyasini na kumwacha katika eneo ambalo aliamini kuwa haitakuwa
rahisi kuonwa kwa mbali na mpitanjia.
Aliporudi garini
alichukua muda mfupi kuifuta michirizi michache ya damu akitumia tambara bovu
alilolikuta humohumo.
Sura yake ikiwa imeshabadilika na
kutangaza bayana kuwa yu tayari kwa lolote, liwe la shari au heri, aliketi nyuma
ya usukani na kulitia gari moto.
Hakuwa dereva mzuri wa gari,
isitoshe, alikumbuka kuwa dereva yule alimwambia kuwa kulikuwa na lita kama kumi
tu hivi za mafuta, hivyo hakutaka kujidanganya kuwa kulitumia gari hilo kutakuwa
na maana yoyote. Ni dhahiri kukamatwa kulikuwa wazi.
Hakufika hata
Kibaha, alilitelekeza kwenye kijiji kimoja na kupata usafiri wa basi lililokuwa
likielekea Dodoma. Saa 11 jioni akawa ndani ya Mji wa Dodoma, mji aliouzoea na
kuupenda kutokana na hali yake ya hewa.
Usiku huo akaumalizia
mjini hapo. Asubuhi ya siku iliyofuata, alikwenda stesheni kusubiri treni.
Hakutaka kupoteza muda kwa kufuata taratibu za upatikanaji wa tikiti, aliamua
kusafiri ‘kimagumashi’ hadi Kigoma.
Treni ilipowasili aliingia
katika behewa la vinywaji na
vyakula.
*******
MARA tu baada ya Temba na
Mado kutoa taarifa katika kituo cha Polisi cha Magomeni, mkuu wa kituo hicho
aliwasiliana haraka na Kituo Kikuu ambako aliongea na Inspekta Banda na kumpa
taarifa hiyo.
Ilikuwa ni taarifa iliyomshtua na kumshangaza
sana Inspekta Banda, lakini pia ikimpa matumaini ya kulipatia ufumbuzi suala
hilo. Papohapo akamhoji mkuu wa kituo cha Magomeni: “Vijana hao waliokupa
taarifa bado uko nao hapo kituoni?”
“Wapo,” Mkuu wa kituo cha
Magomeni alijibu na kuongeza, “Nadhani vichwani mwao wanaziwazia milioni
kumi.”
Kicheko cha dhihaka kikamtoka Inspekta Banda. “Yaani
wanataka kutajirika kupitia kwa Shaka?”
“Labda.”
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ok, utusubiri, baada
ya muda mfupi tutakuwa hapo.”
Dakika chache baadaye, Inspekta
Banda na Sajini Kessy walikuwa ndani ya gari dogo lisilokuwa na nembo ya Jeshi
la Polisi wakielekea Magomeni.
“Shaka ametugeuza mabwege sisi
wote; Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi,” Banda alisema kwa hasira wakati
gari likiteleza kwa kasi katika Barabara ya Morogoro. Kisha akaongeza, “Safari
hii nikimtia machoni nitamshindilia risasi kwa hasira. Hatuwezi kukosa la kusema
kwa vyombo vya habari kuhusu kifo chake. Ni kwamba alijaribu kutoroka wakati
akiwa chini ya ulinzi. Basi!”
“Kwa kweli ni jitu la ajabu
sana,” hatimaye Kessy alisema. “Kinachonishangaza ni jinsi alivyowatoka askari
pale Keko. Hivi afande, inakuingia akilini kuwa Shaka
alitoroka?”
“Una maana gani?” Inspekta Banda alimtazama kessy
kwa macho makali.
ITAENDELEA
0 Comments:
Post a Comment