Simulizi :
Mtikisiko Wa Hirizi
Sehemu Ya Tatu (3)
“N’na maana
kuwa Shaka hakutoroka. Aliruhusiwa kuondoka!”
“Aliruhusiwa?
Aliruhusiwa na nani?”
“Hilo ni jambo lingine. Lakini mimi
binafsi hainiingii akilini kuwa Shaka alitoroka. Atatoroka vipi chini ya ulinzi,
akiwa ni mtu mwenye rekodi mbaya sana anayepaswa kuchungwa kama mtu yeyote
anavyoichunga mboni ya jicho lake?”
Inspekta Banda
aliguna.
“Unasikia afande,” Kessy aliendelea. “Shaka
alihukumiwa jela akiwa ni mtu hatari, jambazi sugu ambaye vyombo vyote vya dola
vinamtambua. Pale Keko wanamjua vizuri Shaka. Walimpokea wakiwa wanamjua vizuri.
Kwa vyovyote, walipaswa kumchunga vilivyo.”
“Lakini nadhani
hujaisahau ripoti ya kutoweka kwake pale gerezani,” Banda alisema. “Shaka
aliondoka katika mazingira ya kutatanisha…”
“Kutatanisha vipi
afande wakati inasemekana kuwa yule askari aliyekuwa na kundi la wafungwa
alibaki ameduwaa tu wakati Shaka akiondoka taratibu?” Kessy alikuwa
king’ang’anizi.
“Kwa hiyo unataka kusema kwamba kulikuwa na
njama za kumtorosha?”
“Ndivyo picha
inavyojionyesha.”
“Ok, lakini hilo silo jambo linalotuhusu kwa
sasa,” Banda alisema. “Twende kwanza Magomeni. Ni huko tutakapopata la
kufanya.”
Walipofika Magomeni na kuwahoji Mado na Temba
wakapata picha ya matumaini. Wakatoka.
“Anaweza kuwa yeye?”
Kessy alimuuliza Banda wakati akiondoka hapo kituoni.
“Ndiye,”
sauti ya Inspekta Banda ilikuwa kavu. “Niliepuka kusema hivyo mbele ya wale
vijana ili kuepusha usumbufu ambao wangetupa. Kwa vyovyote wangetaka kujua
watazipataje milioni zao kumi.”
Kicheko kikamtoka Kessy.
Akauliza, “ Wana ndoto za milioni kumi kabla hata mtuhumiwa
hajapatikana?”
Inspekta Banda
hakujibu.
********
SHAKA alitambua fika kuwa
alipaswa kuwa makini dhidi ya askari, hivyo alipoingia ndani ya treni, alikwenda
moja kwa moja kwenye behewa la vinywaji na vyakula. Huko aliketi na kuagiza
chupa ya maji lita moja. Akatulia kitini akinywa taratibu.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hadi treni ilipofika
kituo cha Saranda hali ilikuwa shwari. Kituoni hapo akashuka na kuagiza kuku na
viazi mbatata kisha akarudi behewani. Akiwa na miwani yake mieusi usoni, miwani
ambayo hakuwa tayari kuitoa bila ya sababu muhimu, huku kofia ikiwa imeganda
kichwani pake, Shaka alianza kukifakamia chakula hicho kwa pupa na baada ya
dakika chache tu zoezi hilo likawa limehitimishwa.
Akaingiza
mkono mfukoni na kutoa noti zilizokuwamo. Alipozihesabu, akafarijika. Zilikuwa
ni pesa za kumtosha kiasi. Kwa kiwango hicho hakuiona sababu ya kumfanya
ashindwe kunywa bia mbili, tatu katika kuiliwaza akili yake kama alivyoamini.
Saa moja baadaye koo likawa limeshateremsha bia mbili. Akaongeza ya
tatu.
Hadi treni ilipokuwa inaingia Tabora, bia tano zilikuwa
zimeshatua tumboni mwake na kuichangamsha akili yake. Naam, kwa kiasi fulani
alijihisi kuwa timamu kisaikolojia huku pia akijali kuwa makini katika maongezi
na mtu yeyote.
Kwa jumla hakutaka kuzoeana na yeyote kwa kiwango
kikubwa, na hilo alilifanya kwa kuwa hakumwamini yeyote kwa kipindi
hicho.
Aliendelea kukaa humo katika behewa la vinywaji na maakuli hadi
saa 7 usiku. Na wakati huduma ilipositishwa na wateja kutakiwa kuondoka, yeye
alimwita mmoja wa wahudumu wa behewa hilo na kunong’ona naye pembeni. Muda mfupi
baadaye kijana huyo alikuwa na shilingi 5,000
kibindoni.
“Us’konde mwanangu,” Shaka aliambiwa. “Pumzika humu
hadi kunakucha. Na kama unataka bia unaweza kuendelea
kuagiza.”
Alichohitaji Shaka siyo kuendelea kukaa humo ili
anywe bia, hapana. Shida yake ilikuwa ni kupata nafasi ya kulaza mbavu hadi
kunakucha. Kama angekuwa na pesa za kutakata asingesita kuonana na TT na kumpa
nauli ya chumba cha daraja la kwanza. Baada ya hapo angemtafuta ‘mrembo’, kati
ya ‘warembo’ wengi wanaozagaa-zagaa ndani ya mabehewa, na ‘mrembo’ huyo
angeifanya safari kuwa fupi kuliko ilivyo.
ASUBUHI ya siku
iliyofuata treni iliingia Kigoma mjini. Na kama alivyokuwa makini safarini, hata
pale stesheni Shaka hakupachukulia kwa uzito wa kawaida. Alijua fika kuwa askari
nchi nzima watakuwa na taarifa kuhusu yeye, hivyo watakuwa wakimsaka kama gaidi
au haini.
Hadhari ikapewa kipaumbele. Akatulia behewani
akiwaacha wenye haraka zao wateremke, yeye akawa miongoni mwa wachache wa
mwisho. Na alipoteremka alikwenda moja kwa moja kukodi teksi moja kati ya nyingi
zilizokuwa zimefurika mbele ya jengo la kituo hicho.
Teksi hiyo
haikumpeleka mbali, alipofika mbele ya soko kuu aliteremka na kumtupia dereva
shilingi 3,000. Kwa hatua ndefu akaingia katikati ya soko ambako alizunguka hapa
na pale bila ya sababu maalumu kisha akatokea upande wa pili, jirani na Benki ya
Taifa ya Biashara ambako alikodi teksi nyingine.
Muda
alioutumia tangu kuachana na ile teksi ya kwanza, kuzunguka ndani ya soko hadi
kukodi teksi ya pili, hazikuzidi dakika tatu, na alifanya hivyo katika kuchukua
hadhari dhidi ya hatari yoyote ambayo ingemnyemelea.
Dakika
kumi baadaye alikuwa akiteremka kwenye makutano ya Barabara za Lumumba na
Mwembengoma, kitongoji cha Mwanga. Kutoka hapo alipita hapa na pale akielekea
nyumbani, Mtaa wa Mabatini.
Alipofika nyumbani wazazi wake
walishtuka lakini wakampokea kwa furaha.
“Kuna msukosuko wowote
uliokupata?” Mzee Songoro alimuuliza wakati wameketi
sebuleni.
“Hapana, sijapata msukosuko wowote,
baba.”
“Nilijua,” Mzee Songoro alisema. “Nilijua tu kuwa
hutapata matatizo yoyote. Sasa tulia. Najua Polisi wanahaha kukutafuta. Wanajua
wewe ni mzaliwa wa hapa Kigoma. Kwa hiyo hata polisi wa hapa watakuwa
wameshapewa taarifa ili wakusake. Lakini hilo lisikutishe. Dawa yao ninayo. Mimi
ndo Songoro mzaliwa wa Tongwe. Hapa ni maji marefu.”
Asubuhi ya
siku iliyofuata Mzee Songoro aliamka mapema, akaenda kituo cha Mwembetogwa
ambako alipanda basi lililomfikisha katika ule msitu ambao alikwenda siku moja
kabla hajafunga safari ya kwenda Dar es Salaam ‘kumkomboa’
Shaka.
Huko aliutafuta mti mwingine na alipoupata, aliuparua
magamba, akayachuma majani na kuyafutika kwenye mkoba. Ni hilo tu lililompeleka
huko. Kilichofuata ni kurudi kando ya barabara kuu ambako zilimchukua dakika
chache tu kupata usafiri wa basi lililomrudisha mjini.
Akiwa
nyumbani aliyachemsha majani na magamba hayo kwa moto mwingi hadi yakalainika
kwa jinsi alivyotaka. Rangi ya maji yale nayo ilibadilika na kuwa nyekundu
kupindukia.
Kazi hiyo ilipokamilika alimwita mwanaye, chumbani
na kumwambia, “Mambo tayari. Vua nguo zote ulale hapo kwenye
mkeka.”
Shaka alitii agizo hilo. Mzee Songoro alitwaa kitambaa,
akachovya ndani ya yale maji yaliyochanganyika na majani pamoja na magamba kisha
akaanza kumkanda mwilini. Maumivu makali yalipenya maungoni mwa Shaka kiasi cha
kumfanya atoe miguno mizito.
“Jikaze! Vumilia mwanangu,” Mzee
Songoro alimwambia. “Hili ndilo zoezi la mwisho katika kuiimarisha kinga yako.
Vumilia, we’ ni mwanamume! Jikaze!”
CHANZO
: http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kazi hiyo
iliendelea.
Baada ya kumkanda mwili wote, mzee Songoro alitwaa
wembe, akamtia chale mikononi, miguuni, kifuani, tumboni, shingoni na kwenye
paji la uso. Kisha alimpaka unga mweusi katika chale hizo huku akinong’ona
maneno fulani ambayo hayakufika masikioni mwa Shaka.
Likafuata
agizo lingine: “Sasa vaa nguo zako, halafu kasimame pale
juani.”
Wakati Shaka akiwa pale juani, Mzee Songoro alikifuata
kivuli chake, akachota mchanga kidogo na kuuchanganya na unga mweusi uliokuwa
kiganjani mwake. Kwa mara nyingine akanong’ona maneno machache huku akimwagia
mchanganyiko huo wa mchanga na unga mweusi toka kichwani hadi
nyayoni.
“Kazi imekamilika,” hatimaye alimwambia huku
akimkabidhi hirizi. “Hii hirizi uivae kiunoni. Na hakuna kuoga hadi jua
litakapozama. Dawa hii inatakiwa kupenya vizuri mwilini, hivyo usikiuke haya
maagizo ninayokupa. Umenielewa?”
“Ndiyo, nimekuelewa, baba,” Shaka
alijibu kwa unyenyekevu.
********
TAARIFA
kuhusu maiti iliyokutwa mtaroni, kando ya Barabara ya Morogoro, kilometa chache
kabla ya kufika Kibaha, ziliyafikia masikio ya Inspekta Banda na mwenzake,
Sajini Kessy saa saba mchana wakati wakiwa ofisini katika Kituo Kikuu cha Polisi
jijini Dar es Salaam. Muda mfupi baadaye zikapatikana taarifa za kutambuliwa kwa
maiti hiyo.
Baada ya taarifa ya kutoweka kwa mfungwa katika
gereza la Keko siku iliyopita, mfungwa aliyekuwa na sifa ya kutenda uhalifu
mkubwa hata kutoa roho za watu, akili ya Inspekta Banda ilizama kwa mtu mmoja
tu; Shaka Songoro!
Hadi kufikia siku hiyo, hakuwa na tetesi
zozote kuhusu ni wapi atakakokuwa Shaka, lakini alijenga imani kuwa lazima
atakuwa kwenye mpango wa kulikimbia jiji. Hivyo, hata alipokuwa meza moja na
Sajini Kessy, hakusita kuziweka bayana hisia zake. “Kwa vyovyote huyo atakuwa ni
Shaka tu,” alisema.
“Kwa nini unadai hivyo, afande?” Kessy
alimuuliza.
Banda alikohoa kidogo kisha akasema, “Inasemekana
marehemu alikuwa ni dereva teksi. Na alitoka Magomeni akiwa na abiria mmoja
aliyevaa kofia pana kichwani na miwani myeusi usoni.
“Madereva
wa pale Magomeni wanadai kuwa marehemu aliondoka na abiria huyo kitu kama saa
tatu hivi, asubuhi. Hakurudi tena hadi ilipokuja kupatikana maiti
yake.”
“Lakini afande,” Kessy alisema na kusita. “Wale vijana
wa gesti wanasema mpangaji wao anafanana sana na huyu mtu,” akamwonyesha picha
ya gazetini. Kisha akaendelea, “Na hao madereva wanadai kuwa huyo abiria alivaa
kofia na miwani myeusi. Huoni kuwa hao ni watu wawili
tofauti?”
“Wanaweza kuwa watu wawili tofauti au ni mtu
yuleyule,” Inspekta Banda alisema. “Kumbuka, yule ni jambazi sugu na mkongwe.
Unadhani atakuwa mjinga kiasi gani, aiache sura yake hadharani huku akitambua
fika kuwa anasakwa? Hawezi kuwa bwege kiasi hicho. Kwa vyovyote lazima atapitia
dukani ambako atapata kofia na miwani kwa nia ya kuubadili mwonekano wake kwa
watu. Au atafanya chochote kile katika kuhakikisha hatambuliki kwa urahisi kwa
watu. ”
Kessy aliyatafakari maneno hayo ya Banda na kwa kiasi
fulani akajiona yu mpumbavu kwa kutolitambua hilo mapema kabla hajatamka
chochote.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hatashindwa!” Inspekta
Banda alisisitiza. “Shaka siyo chizi. Ana akili timamu. Lazima afanye mambo yake
kwa mpangilio, umakini na kwa tahadhari kubwa. Ni mhalifu mwenye uzoefu na kazi
yake!”
“Kwa hiyo, afande, operesheni yetu ilenge kumsaka Shaka
pekee?”
“Shaka nd’o apewe kipaumbele huku upelelezi zaidi
ukiendelea.”
******
SHAKA aliupenda uhuru. Na
alipenda kuutumia uhuru huo kwa starehe. Pesa zilipojikita mifukoni mwake, pesa
zinazoweza kumtia kiburi, alipenda kuingia kwenye kumbi za dansi kuburudishwa na
muziki na kujistarehesha kwa vinywaji.
Si hayo tu, bali pia ni
pesa hizo zilizompa kiburi cha kuwadaka wanawake warembo ambao walijua ni kipi
cha kumfanyia mwanamume mkware, apendaye kujistarehesha na wanawake
watundu.
Ndiyo, aliuzoea mfumo huo wa maisha akiwa jijini Dar
es Salaam, jiji aliloamini kuwa ni kitovu cha maraha Tanzania. Lakini
alifanikiwa kuponda raha hizo pale tu pesa zilipofurika mifukoni
mwake.
Siku tatu za mwanzo akiwa mjini Kigoma alijiona kama
vile yu jehanamu. Zile starehe alizozipenda na alizozizoea hakuzipata. Na
hakuzipata kutokana na ukosefu wa pesa. Akiba pekee aliyokuwa nayo haikuzidi
shilingi 10,000. Kwake, hizo hazikuwa ni pesa za kumfanya ajisikie yu miongoni
mwa wanaume duniani. Ataingia baa kufanya nini akiwa na vijisenti hivyo?
Ataupata wapi ujasiri wa kuzungumza na mwanamke mzuri akiwa na kiwango hicho
kidogo cha pesa?
Hivyo hakutaka kuendelea kutaabika,
aliamua kutumia mbinu zake alizozizoea ili apate pesa zaidi. Ndipo alipoanza
kuvinjari kwenye vibanda vya gongo ambako zaidi ya kuuza pombe hiyo pia
zilipatikana bia za Tanzania hata za Burundi na Kongo.
Aliingia
katika nyumba hizo akiwa ni mteja wa bia na watu wakampapatikia hususan wale
wanywaji wa gongo ambao aliwanunulia chupa moja ya ‘fanta’ iliyotosha
kuzichangamsha akili zao huku yeye akinywa bia taratibu.
Ni
katika nyumba moja kati ya tatu alizoingia ndiyo aliyoiona inafaa kwa malengo
yake. Japo ndani ya nyumba hiyo kuliuzwa gongo na bangi, hata hivyo isingekuwa
rahisi kwa mtu wa kawaida kubaini hivyo. Wateja wake walikuwa ni ‘wastaarabu,’
wasiopenda kelele wala kulewa sana.
Isitoshe, mandhari ya
sebule ambayo wateja waliitumia ilikuwa ni ya kuvutia. Pangaboi kubwa darini
lilizunguka kwa nguvu muda wote na kuifanya hewa ya humo ndani kuwa nzuri. Pia
kulikuwa na televisheni kubwa iliyowaburudisha wateja waliokuwa wameketi kwenye
masofa ya kuvutia.
Kwa aliyehitaji kuvuta bangi aliwasiliana na
muuzaji na alipopewa msokoto, alikwenda katika vyumba vya uani ambako ‘alipata
stimu’ bila ya kuwakera wasiovuta.
Siku yake ya kwanza katika
nyumba hiyo alipata marafiki wawili. Siku ya pili alikuwa na marafiki watatu.
Kwa kuwatumia marafiki hao akafanikiwa kuwajua watu wawili wa mjini hapo,
alioamini kuwa angeweza kupata pesa kwao iwe kwa hiari yao au kwa shinikizo
lake!
Mmoja wa ‘matajiri uchwara’ hao aliishi Kibirizi Road na
mwingine alikuwa Lumumba Road. Hazikupita siku tatu kabla ya watu hao
hawajakutwa wamekufa kwa majeraha ya visu, mmoja kisu cha shingoni na mwingine
cha kifuani.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni kazi
yake!
Kwa Mji wa Kigoma, kutokea mauaji ya watu wawili kwa siku
moja, tena yakiwa ni mauaji ya kikatili, na waliouawa wakiwa ni watu maarufu,
ilikuwa ni habari kubwa na ya kushtua moyo wa kila mwenye akili
timamu.
Yalikuwa ni matukio yaliyoitikisa Kigoma kwa kiasi
kikubwa. Jeshi la Polisi likaingia kazini. Ikawa ni operesheni kubwa na ngumu.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Katembo Shabana akamwamuru mkuu wa kitengo cha
uchunguzi kulivalia njuga suala hilo sanjari na kuhakikisha kuwa ulinzi wa
mipakani unaimarishwa.
“Sidhani kama mauaji haya yanaweza kuwa
yamefanywa na majambazi wa Kitanzania,” Katembo alimwambia mkuu wa kitengo cha
uchunguzi. “Sidhani. Hawa wanaweza kuwa Warundi au Wakongo. Itatubidi tuwe
serious kwa suala hili.”
********
KUUA,
hususan kuua mtu, halikuwa jambo la ajabu kwa Shaka. Alishaua zaidi ya watu saba
katika historia ya maisha yake. Na alikuwa tayari kufanya hivyo wakati wowote na
dhidi ya mtu yeyote kwa dhamira ya kupata pesa. Katika utekelezaji wa hayo
majukumu yake ya kuua, silaha zake kuu zilikuwa ni visu na
bastola.
Baada ya kuwaua wale watu wawili, alijua kuwa lazima
Jeshi la Polisi litakuwa katika operesheni kubwa ya kumsaka mhusika wa matukio
hayo. Na operesheni hiyo lazima imguse yeye kwa kuwa hata kitendo chake cha
kutoroka kule gerezani, Keko, kitawafanya Polisi jijini Dar wamfuatilie hadi
hapo Kigoma.
Matukio haya ya vifo vya watu wawili yatawafanya
askari wamshuku yeye kwa asilimia mia moja. Hivyo alipaswa kuwa makini na
kujiwekea ulinzi madhubuti japo baba yake alimwambia kuwa tayari ana kinga nzuri
dhidi ya hatari yoyote.
Alihitaji kuwa na bastola, lakini
ataipata wapi? Hakuwa na jibu. Na alipotafakari zaidi akaona uwezekano wa kupata
bastola haupo. Hivyo akaamua kujichimbia ndani mchana kutwa na kutoka usiku tu,
akienda katika baa zilizotulia ambako alijipatia bia mbili, tatu na kurejea
nyumbani.
Hata hivyo, japo alishindwa kuutumia uhuru wake kwa
kustarehe bila ya wasiwasi, bado hakuacha kuwachukua kina dada, mmoja baada ya
mwingine kwa siku tofauti na kwenda nao nyumbani, chumbani mwake ambako
aliupitisha usiku akiburudika.
Matukio yale ya mauaji ya watu
wawili yalimwingizia shilingi 1,700,000 tu pesa ambazo hazikuwa za kumfanya
yeyote mwenye kuhitaji pesa za kutanulia ajione kuwa sasa
kapata.
Hata hivyo, pamoja na uchache huo wa pesa hizo, kwa
kiasi fulani alijiona yu mwanamume kati ya wanaume; anaweza kuvuta sigara huku
akili imetulia, anaweza kunywa bia kwa kujidai na anaweza kujipatia mwanamke
mwenye mvuto mkali na ‘kumhukumu’ apendavyo.
Kwa siku tatu
mfululizo alikuwa mtu wa kutoka nyumbani giza linapoingia, bila ya kujali kuwa
kwa kufanya hivyo alikuwa akilipunguza pato lake taratibu huku akiwa hana
uhakika wa kuliongeza kwa mbinu gani, kupitia kwa nani na wakati
gani.
Siku ya nne alikwenda katika baa ileile aliyokwenda tangu
majuzi. Ni Bigabiro Bar iliyokuwa Mtaa wa Kitambwe. Na siku hii hakutaka
kuchelewa sana katika baa hiyo. Alipanga kuwasiliana na mhudumu mmoja aliyeitwa
Mary, ili, kama ilivyokuwa siku iliyopita, usiku huo pia ndiye
amstareheshe.CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa 3.00
alikuwa akiingia ndani ya baa hiyo kwa madaha, shilingi laki moja na kitu
zilizokuwa mfukoni zikimtia kiburi.
Bia ya kwanza ilipotua
mezani aliinywa taratibu huku akimsubiri Mary, aje, wapange vya kupangika.
Hazikupita hata dakika tano, mara Mary akamjia huku akitembea kwa
madaha.
“Inakuwaje bwana we?” Mary alimuuliza huku
akiutikisatikisa mguu wa kulia.
Mary huyu alikuwa tofauti na
yule Mary wa jana. Alikuwa ndani ya vazi laini ambalo japo halikumbana mwilini
hata hivyo lilimvutia hususan pale alipokuwa akitupa mguu mmoja baada ya
mwingine, akitembea kwa madaha. Umbo lake lililojaajaa liliyavuta macho ya
wanywaji wengi waliofika hapo baa. Na wengi wao hawakukosa kumsumbua kwa maneno
ya kumtaka kimapenzi.
Hata hivyo, hakuwa na tabia ya kuwakubali
kirahisi wateja wanaomtongoza baada ya kufakamia bia. Na zaidi, hakupenda
kuwakubali watu ambao mwanzo wao wa utongozaji ni kutamba kuwa wana pesa nyingi
na pia kumwahidi mambo mengi mazuri, ahadi ambazo alitambua fika kuwa ni uongo
mtupu.
Pia, baadhi yao walikuwa na tabia ya kutamka matusi ya
nguoni na kumtania kwa kiwango kikubwa, utani usiopendeza, wakionyesha kuwa
mwanamke yeyote anayefanya kazi ya uhudumu wa baa ni
malaya.
Alimkubali Shaka kwa kuwa kwanza, aligundua kuwa ni
mgeni wa eneo hilo, na pili, alimwona kuwa ni mtu ambaye hakuwa na marafiki
ambao huenda wakamshawishi aachane na wanawake wa baa.
“Kama
jana,” Shaka alimjibu huku macho yakimkagua kutoka juu mpaka chini. Kisha
akaongeza, “Au leo una miadi na mtu mwingine?”
“Nani huyo?”
Mary alijitia kukunja uso kama aliyekerwa na swali la Shaka. Kisha akavuta kiti
na kuketi jirani naye. Akamtazama usoni sawia, kisha huku akiibinua-binua midomo
yake kwa madaha na kuichezesha pua yake kwa maringo, akamuuliza, “Hivi
unanionaje? Unaniona mie malaya sana, sio? Yaani kufanya kazi ya baa nd’o
umeniona kuwa mimi ni maharage ya Mbeya?”
Shaka alitabasamu
kidogo na kumpigapiga begani Mary. “Basi, beibe. Nakutania tu. Acha kuhamaki.
Yaani hutaniwi hata kidogo?”
“Bwana, utani mwingine s’o mzuri,”
Mary alisema kwa deko huku akimpapasa Shaka kidevuni. Kisha mkono huo ukahama na
kushuka kifuani ambako vifungo kadhaa vya shati la Shaka havikuwa vimefungwa.
Akampapasa na kuzitomasa chuchu zake.
Shaka akaguna na
kuutoa mkono huo kistaarabu. Lakini Mary hakutulia, papohapo akaushusha mkono
hadi chini ya kitovu ambako ulifanya kile kilichomchanganya zaidi Shaka.
Alitomasa kwa namna ya kipekee na kumshuhudia Shaka akihema kwa
tabu.
Hata hivyo, Mary alijua kuwa hapo hapakuwa mahali
palipostahili kwa michezo ya aina hiyo. Akautoa mkono na kuketi
kistaarabu.
“Si utanisubiri?” hatimaye alimuuliza Shaka kwa
sauti ya chini.
“Mpaka saa ngapi?”
“Leo
tunafunga saa tano.”
“Poa tu. Mimi sina noma, muda unaniruhusu.
Na leo hakuna kulala.”
“Wewe tu, mie niko ngangari kwa saa
ishirini na nne. Pumzi yako
tu.”
“Tutaona.”
“Sawa, tutaona,” Mary alisema
huku akinyanyuka na kuondoka kwa madaha yaleyale, umbo lake likiendelea kuyavuta
macho ya watu kwa mitikisiko yake.
Shaka akaagiza bia ya
pili.
*********
KITENGO cha Upelelezi cha
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma, kilimtumia Kisu katika operesheni ya kumsaka
Shaka baada ya kupatikana taarifa kutoka Dar es Salaam kuwa jambazi huyo ambaye
ni mzaliwa wa mjini Kigoma alitoroka gereza la Keko katika mazingira ya
kutatanisha.
Ni kwa kushuku kuwa huenda Shaka akawa
amejichimbia hapo mjini Kigoma, ndipo walimhusisha na mauaji ya wale watu
wawili, mauaji ambayo kwa mtazamo wao hayawezi kufanywa na mtu asiyekuwa mzoefu
kwa vitendo vya kikatili.
Kisu akiwa ni kachero aliyeaminika
sana kwa wakuu wake wa kazi, alihaha kwa siku mbili mfululizo bila ya mafanikio
ya kupata walao fununu za kuweza kumsaidia. Ni siku ya tatu, saa tano asubuhi
ndipo alipopata taarifa ambazo kwa kiasi fulani aliona kuwa zingeweza
kumsaidia.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwamba, mtu mmoja
alionekana katika baa moja akitamba kuwa hakuna wa kumsumbua iwe kwa ngumi au
silaha ya moto.
“Mimi ni mtoto wa town, ukiniletea umbulula
wako nakutoa roho ka’ vile sikujui daaadek…!”
Ni kauli hiyo, na
nyingine nyingi zifananazo na hiyo ndizo zilizomfanya kijana mmoja amtilie shaka
na hivyo kupata nguvu ya kukimbilia kwa kachero Kisu ambaye walifahamiana kwa
muda mrefu.
Kisu, akiwa bado yu gizani katika operesheni ya
kumsaka mtuhumiwa wa vifo vya watu wawili na wakati huohuo akiwa pia katika
zoezi la kumsaka Shaka, ambaye kwa mujibu wa taarifa kutoka Dar huenda akawa
kakimbilia hapo Kigoma kwa kuwa ndiko alipozaliwa, hakutaka kuipuuzia taarifa
hii aliyopewa na huyu kijana.
Saa tatu usiku aliingia ndani ya
baa hiyo na kukuta idadi ya watu ikiwa kubwa tofauti na alivyopazoea.
Hakushangazwa na wingi huo wa wateja. Kulikuwa na sababu. Tarehe. Ndiyo, siku
hiyo ilikuwa ni tarehe 31, ikiwa ni siku ya mwisho kabisa ya mwezi huo, hivyo
aliamini kuwa watu wengi walioajiriwa walikuwa wamepata mishahara yao na kuamua
kuja hapo na sehemu nyingine ‘kujipongeza.’
Yeye hakujali hilo,
alijali kilichomwingiza humo. Akaangaza macho huku na kule akitafuta sehemu
nzuri ya kukaa. Na alipoipata alivuta kiti na kuketi kisha akaagiza
kinywaji.
Katika meza aliyokuwapo pia kulikuwa na mtu mmoja,
mwanamume ambaye alionekana kukolewa vilivyo na kilevi. Hakumjali, akawa katika
zoezi la kuangaza macho kwa takriban kila aliyekuwemo.
Dakika
chache baada ya kulianza zoezi hilo, macho yaliganda kwa mtu mmoja, mwanamume
pandikizi ambaye alikuwa ameketi katika kiti kirefu kilichokuwa kaunta, bia
mbele yake.
Kilichomfanya Kisu amgande mtu huyo ni jinsi
alivyokaa katika eneo hilo. Ulikuwa ni ukaaji wa ajabu, ambao kwa mtu yeyote
mstaarabu usingekuwa wa kupendeza. Alikuwa amepandisha mguu mmoja juu ya kiti
kilichokuwa jirani yake na hivyo kuwa kama aliyezuia mtu yeyote mwingine kuketi
hapo.
Kwa dakika nne, tano hivi ambazo Kisu aliendelea
kumchunguza mtu huyo, aligundua kuwa hata wamiliki na wahudumu wa baa hiyo
hawakuthubutu kumwonya mteja
wao.
********
SIGARA ikivutwa kila baada ya
muda mfupi, kuketi huku guu moja likiwa juu ya kiti cha pili, na kumtomasatomasa
Mary kila alipofika kumpa huduma ya kinywaji ni vitendo ambavyo Shaka alitarajia
kuwa visingewafurahisha wateja wengi katika baa hiyo. Na alitarajia kuwa wengi
wao wangemkodolea macho wakimstaajabia.
Ndiyo, alitarajia
hivyo, lakini hakutarajia kuwa wateja hao wangetekwa na vitendo vyake kiasi cha
kuahirisha mara kwa mara kuzipeleka vinywani glasi zao za
vinywaji.
Mtu mmoja tu kati ya hao wateja alimtilia shaka. Kwa
uzoefu wake katika kazi ya kupambana au kutafutwa na vyombo vya dola hakusita
kumjumuisha mtu huyo na wale ‘askari kanzu.’
Macho ya mtu huyo
yalitangaza bayana uaskari wake! Pia Shaka hakushindwa kung’amua kuwa mtu huyo
yuko hapo kwa sababu maalum na wala siyo kustarehe.
Akilini
mwake aliona kuwa ni mapema mno kwa askari kumfuatilia hadi kuwa hatua chache
kabla ya kumtia mbaroni. Bado alikuwa hajayafaidi maisha, na bado alikuwa
hajazifaidi pesa alizopora kwa wale matajiri wadogo.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hata hivyo alikwishaona
kuwa dudubaya limeingia katika himaya yake. Sasa hakutaka kupoteza muda.
Alikunywa bia yake haraka kisha akatoka. Kwa hatua ndefu na kwa hadhari
alitembea akielekea msalani.
Hakuwa amebanwa na haja ndogo wala
kubwa, aliamua tu kwenda huko ili apate wasaa wa kupanga nini afanye katika
kukabiliana na hali tete iliyokuwa mbele yake. Tayari alishaamini kuwa ujio wa
yule aliyeamini kuwa ni askari sio ujio wa heri, hivyo alipaswa kuwa makini na
ikibidi, achukue hatua haraka iwezekanavyo katika
kujihami.
Akajipapasa mifukoni na kukigusa kisu chake. Ujasiri
ukamjaa. Akakikamata kitasa cha mlango akitaka kurudi
ukumbini.
********
ITAENDELEA
0 Comments:
Post a Comment