MTIKISIKO WA HIRIZI - 1
.jpg)
IMEANDIKWA
NA : INNOCENT A.
NDAYANSE
*********************************************************************************
Simulizi
: Mtikisiko Wa Hirizi
Sehemu Ya Kwanza (1)
SIYO KWAMBA
KILA MWANADAMU ANAAMINI KUWA ILI UTATUE TATIZO LOLOTE LINALOKUKABILI LAZIMA UWE
NA ELIMU YA KIWANGO KIKUBWA, UWE MJANJA WA MJINI AU MCHA MUNGU UTEGEMEAYE
MAOMBEZI KWA KUFANIKISHA MAMBO YAKO. WAPO AMBAO HAWAPO KATIKA MAKUNDI YOTE HAYO.
WAO HUAMINI ZAIDI KATIKA KILE KINACHOITWA ‘NGUVU ZA GIZA.’ KATIKA RIWAYA HII
UTASHUHUDIA MAMBO YANAYOFANYIKA CHINI YA JUA, YAKIWASTAAJABISHA WALE WENYE AKILI
ZA KAWAIDA NA KUWASISIMUA WENYE MIOYO YA KIJASIRI. ANZA
KUTIRIRIKA…
MWAKA
2002
MVUA ya rasharasha iliyoanza kunyesha tangu asubuhi mjini
Kigoma, iliendelea hata usiku ulipotinga. Na hakukuwa na dalili ya kukatika au
kuongezeka. Hilo halikuwa jambo la ajabu kwa kipindi hicho cha masika mvua
kunyesha kwa zaidi ya saa 10. Lilikuwa ni jambo la
kawaida.
Usiku huo, Mzee Songoro alikuwa nyumbani kwake,
itongoji cha Mwanga, Mtaa wa Mabatini akisubiri mlo wa usiku uliokuwa
ukiandaliwa na mkewe. Alikuwa ameketi sebuleni akitazama televisheni huku pia
akisubiri taarifa ya habari.
Ilipotimu saa 2.00 kituo fulani
cha televisheni kikaanza kutangaza taarifa ya habari, muhtasari ukiwa utangulizi
wa habari yenyewe. Kwanza Mzee Songoro alishtuka, kisha akashangaa. Hakuyaamini
masikio wala macho yake. Akatega masikio kwa makini na kukikodolea macho makali
kioo cha televisheni.
Kisha habari kamili
ikaanza:
JAMBAZI SUGU, ALIYETUHUMIWA KWA MAKOSA MBALIMBALI
YAKIWAMO YA UBAKAJI, WIZI WA KUTUMIA SILAHA NA MAUAJI, SHAKA SONGORO, LEO
AMEHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA BAADA YA MAHAKAMA KURIDHIKA NA MAELEZO YA UPANDE
WA MASHTAKA, MAELEZO YALIYOAMBATANA NA USHAHIDI MZITO ULIOMTIA HATIANI
MSHTAKIWA…
Ilikuwa ni habari ndefu iliyoambatana na picha ya
mtuhumiwa huyo. Na ikawa ni habari iliyomshtua na kumsononesha Mzee Songoro kwa
kiasi kikubwa. Hakuendelea kuitazama televisheni hiyo wala kutega masikio
kusikiliza habari nyingine.
Alinyanyuka na kuvuta hatua mbili
akielekea jikoni, lakini mara akasita. Akarudi sofani na kujipweteka
pwaa!
Akashusha pumzi ndefu. Kisha akaita kwa sauti kali: “Mama
Shaka! Mama Shaka weee!”
Ilikuwa ni sauti iliyoyafikia masikio
ya mkewe kwa usahihi, ikamshtua na kumshangaza. Akaacha kufanya alichokuwa
akikifanya. Akaenda sebuleni huku akitweta.
“Vipi, baba
Shaka?”
“Keti,” Mzee Songoro alimwamuru huku kakunja
uso.
“Kuna nini baba Shaka, mbona unaniweka roho juu?” Mama
Shaka alihoji huku akijipweteka sakafuni puu!
Mzee Songoro
hakuwa na pupa ya kuzungumza. Alitulia na kushusha pumzi kwa nguvu. Kisha
akaingiza mkono ndani ya mfuko wa koti lake jeusi na kutoa msokoto wa
tumbaku.
Akauweka mezani na kuingiza tena mkono huo ndani ya
mfuko wa suruali. Huko akatoa kibiriti. Akahema kwa nguvu na kumtupia jicho Mama
Shaka. Akagundua kuwa amekumbwa na woga.
“Tulia,” alimwambia.
“Tulia. Usihofu, Mama Shaka.” Akauwasha msokoto wa tumbaku yake na kuvuta
mikupuo miwili, mitatu kwa nguvu. Muda mfupi baadaye akapuliza moshi angani.
Sasa akayarejesha macho kwa mkewe, Mama Shaka.
“Shaka
amefungwa!” alisema kwa sauti nzito na ya chini sana akionyesha dhahiri kukumbwa
na fadhaa.
“Nini?!” mkewe alitokwa macho pima. “Unasemaje Baba
Shaka?”
“Shaka amefungwa!” Mzee Songoro aliirudia kauli yake,
safari hii kwa msisitizo mkali.
“Nani
kakwambia?”
“Hiyo hapo,” Mzee Songoro alisema huku akimwonesha
mkewe kwenye televisheni. “Wametangaza sasa hivi na nimeiona picha yake kwa
macho yangu haya!” akakielekeza kidole cha shahada usoni pake.
Mama Shaka
alijikunja na kujikunjua pale sakafuni. Akahema kwa shida akiwa hayaamini
masikio yake.
“Unaikumbuka ile kesi iliyokuwa ikimkabili?” Mzee
Songoro alimuuliza.
“Ndiyo, naikumbuka.”
“Basi
ni hiyo iliyomfunga.”
“Mungu wangu! Mwanangu Shaka!” Mama Shaka
aliomboleza. “Mwanangu Shaka kafungwa! Kafungwa miaka
mingapi?”
“Miaka mingapi?” Mzee Songoro alimtazama mkewe kwa
namna ya kumshangaa. Kisha akaongeza, “ Siyo wa kutoka leo au kesho. Ni mpaka
kiama!”
“Mungu wangu!” mkewe aliomboleza tena huku akitokwa
machozi. Akajipigapiga kifuani kwa uchungu. Kisha akauliza, “Una maana
kahukumiwa kifo?”
”Hakuna tofauti na kuhukumiwa kifo,” Mzee
Songoro alijibu. “Hatutakaa naye tena hapa nyumbani tukizungumza. Kuonana kwetu
ni mpaka twende gerezani, na huko mtu unapewa dakika mbili, tatu tu za
kuzungumza naye, tena askari akiwa kando yenu.”
Ulipita ukimya
mfupi, wote wakiwa wamezama mawazoni. Mara Mzee Songoro akaibuka tena, na kwa
msisitizo mkali akasema, “Mama Shaka, siwezi kumwacha mwanangu wa pekee afie
jela. Kwa hilo siko tayari!”
Mkewe aliunyanyua uso na
kumtazama, kisha akauliza, “Sasa utafanya nini Baba
Shaka?”
“Nitajua la kufanya, lakini ni lazima nimwokoe
mwanangu!”
*******
KILIKUWA ni kiapo cha Mzee
Songoro, kiapo alichokitoa kwa dhati, kutoka moyoni mwake. Alfajiri ya siku
iliyofuata aliamka na kutwaa kijimfuko kidogo, cheusi kisha akaondoka. Akachapa
mguu hadi Mwembetogwa ambako alipata usafiri wa basi lililokuwa likielekea
Kasulu. Yeye hakuwa na safari ya Kasulu, gari lilipokipita Kijiji cha Simbo na
kwenda kilometa chache mbele, aliteremka.
Hapo alipoteremkia
hakukuwa hata na nyumba wala dalili ya uhai wa binadamu. Kulikuwa na pori zito.
Abiria wenzake, dereva na kondakta walimshangaa, lakini hawakumdadisi kuhusu
hilo.
Akapenya ndani ya pori hilo, akitembea taratibu huku
akijitahidi kuiepuka miba na kujihadhari na nyoka waliosemekana kulitawala eneo
hilo. Alikuwa makini wakati akilivaa pori hilo, akiangaza macho huku na kule na
kwenye mti huu na ule hadi alipokomea chini ya mti
aliouhitaji.
Akautazama mti huo huku kwa mbali akitetemeka.
Hakuwa akitetemeka kwa hofu, bali alitetemeka kutokana na baridi kali iliyopenya
maungoni mwake. Akafungua ule mfuko wake mweusi na kuchomoa kisu. Akausogelea
mti huo na kuanza kuuparua magamba taratibu na kwa umakini wa hali ya
juu.
Magamba hayo alikuwa akiyaweka ndani ya mfuko huo.
Alipotosheka na idadi ya magamba aliyopata, alianza safari ya kurejea nyumbani,
moyoni akiwa amesuuzika kwa mafanikio ya safari yake.
Alipofika
nyumbani hakuwa na haraka ya kumtaarifu chochote mkewe. Alitulia hadi baada ya
mlo wa usiku ndipo alipomwita na kumwambia, “ Kesho n’taondoka.”
“Sijakuelewa, baba
Shaka,” mkewe alisema huku akiondoa vyombo vilivyotumika kwa
maakuli.
“Kesho n’taondoka!” Mzee Songoro aliirudia kauli yake,
safari hii kwa msisitizo. “Nakwenda Dar kumkomboa
mwanangu.”
“We baba Shaka, utamkomboaje mwan’etu?” Mama Shaka
aliuliza huku akiacha kufanya kila alichokuwa akikifanya. Akasimama wima na
kumtazama mumewe kwa mshangao, mikono kaikita kiunoni.
“Hayo
nitayajulia hukohuko,” Mzee Songoro alisema. “Lakini kwenda ni lazima. Nina
hakika Shaka hataendelea kusota gerezani, labda mimi nisiwe Songoro niliyezaliwa
Tongwe na kukulia Kasingirima Ujiji kabla ya kuja kujenga huku
Mwanga.”
Naam, Mzee Songoro hakuwa na mzaha kuhusu suala hilo.
Alidhamiria kumtoa mwanaye kifungoni, iwe, isiwe.
Asubuhi ya
siku iliyofuata alikwenda Stesheni na kuonana na mtu mmoja, mfanyakazi wa
Shirika la Reli ambaye alimpatia tikiti ya Daraja la Tatu ya kumtoa Kigoma hadi
Dar es Salaam.
Kisha alirudi nyumbani na kuanza kujiandaa rasmi
kwa safari hiyo ya dharura. Alikwenda kwenye duka la jirani ambako alinunua
chupa ya maji yenye ujazo wa nusu nusu lita, akaweka akayanywa maji kidogo mbele
ya muuza duka kisha akaondoka na mbele kidogo akayamwaga maji
yaliyosalia.
Kwa kujidai akaenda nyumbani ambako alitwaa yale
magamba aliyoyatoa porini jana yake na kuanza kuyaponda.
Zoezi
la kuyaponda magamba hayo lilidumu kwa takriban nusu saa hadi yakalainika na
kupatikana unga ambao ndio ulikuwa muhimu kwake. Akautwaa unga ule na kuumimina
kidogo ndani ya chupa ile ya maji. Unga mwingine aliuweka ndani ya kijichupa
kidogo. Kisha alitwaa mzizi, akauzungushia karatasi na kuuweka kando ya ile
chupa ya maji.
Baada ya kufanya hiki na kile katika maandalizi
hayo, hatimaye alijipweteka sofani na kupumua kwa nguvu. Akaisumbua akili yake
kufikiri ni kipi cha muhimu ambacho huenda amekisahau. Dakika mbili, tatu
alizotulia zilitosha kumfanya aamini kuwa hakukuwa na kitu chochote kingine
kilicho muhimu katika safari hiyo ambacho amekisahau.
NDIPO
akamwita mkewe na kumwonya, “Uwe mwangalifu na vijizi vinavyozurura usiku kucha
kwenye majumba ya watu. Sitarajii kuchukua zaidi ya siku tatu kule Dar. Na kama
sitarudi na Shaka, basi nitahahakisha kuwa namwacha katika mazingira mazuri ya
kurudi uraiani ndani ya siku saba tu. Lazima kifanyike
kitu.”
“We Baba Shaka!” mkewe alisema huku akijishika shavu kwa
mshangao. Kisha akaongeza, “Una hakika na hayo
unayon’ambia?”
“Naamini Mungu atanisaidia. Najua mwan’etu,
Shaka anapata pesa kwa njia ambazo dini mbili kubwa duniani, Uislamu na Ukristo
haziafikiani nazo. Ni mwizi! Tuseme ni jambazi! Ukweli ndio huo! Lakini sisi
tunatakiwa kujali kuwa ni mwan’etu. Ni damu yetu. Ni mwanangu, ni mwanao!
Umenielewa?”
“Nimekuelewa kidogo.”
“Siyo
unielewe kidogo, unielewe sana!” Mzee Songoro alifoka. “Yule ni mtoto wetu!
Tunapaswa kumwokoa. Pesa alizokuwa anatutumia ndizo zimefanikisha kupata hii
nyumba. Yeye halijui hilo! Hivi unadhani koo na familia mbalimbali zinashamiri
vipi mitaani na kuonekana kuwa wameendelea? Unadhanai watu wanaendelea kilahali
tu? Na siku hizi nd’o mambo yamezidi hasa kwa hao wanaowaua wanadamu wenzetu;
albino….dah…
“Sijui dunia inakwenda
wapi…lakini tuachane na hao washenzi was’ojali uhai wa wanadamu wenzao, mimi
nazungumzia mapenzi yangu kwa mwanangu. Yeye hachuni ngozi, hamtafuti albino,
hamtafuti mtu mwenye upara wa asili…mwanangu ni tofauti mama Shaka! Yeye anasaka
pesa kivyake! Akikuotea, unaye!”
Mzee Songoro akasitisha
kuzungumza, akahema kwa nguvu na kumtazama mkewe kwa jicho kali, jicho
lililomtisha mama Shaka.
“Basi, baba Shaka,” Mama Shaka
alimkatiza. “Nimekuelewa Baba Shaka. Nenda…nenda ukamwokoe mwan’etu.
Nenda!”
********
TRENI ya abiria iliondoka
mjini Kigoma saa 11.00 jioni. Siku ya pili Mzee Songoro alikunywa chai mjini
Tabora saa 12.30 alfajiri. Mchana huo akasota ndani ya treni hiyo hadi jioni
alipotinga ndani ya Mji wa Dodoma. Siku ya tatu, saa nne asubuhi aliingia jijini
Dar es Salaam.
Hakuwa mgeni wa jiji hilo. Mara kadhaa kwa miaka
kadha wa kadha iliyopita alikuwa akifika katika jiji hilo kwa shughuli zake
binafsi au kwa kutembelea ndugu, jamaa na marafiki.
Kwa hali
hiyo, hakupata shida kutafuta usafiri wa kumfikisha Magomeni Mapipa. Kwanza
alitembea taratibu hadi eneo la Mnazi Mmoja katika kituo cha ‘Baridi’ na hapo
alisubiri kwa dakika chache tu kabla hajapata usafiri wa
daladala.
Alipofika Magomeni alikodi teksi iliyompeleka katika
gesti moja ambako alichukua chumba na kuanza kupanga hatua moja baada ya
nyingine katika kazi iliyomkaabili, kazi ngumu lakini aliyoamimi kuwa
isingemshinda.
********
JUMAPILI asubuhi, hii
ikiwa ni siku ya pili baada ya kuingia jijini Dar es Salaam, Mzee Songoro
aliamka mapema, akaoga na kupata stafutahi katika mgahawa uliokuwa jirani na
gesti hiyo.
Mazingira ya hali ya hewa ya jiji hilo yalimpa
shida lakini alivumilia. Japo ndiyo kwanza ilikuwa ni saa 1.30 asubuhi, hata
hivyo alihisi joto kali mwilini tofauti na hali ya hewa ya Kigoma. Alikunywa
chai kwa kuwa tu ilimlazimu afanye hivyo kutokana na njaa kali iliyomsakama
tumboni.
Alipomaliza alitoka huku akijifuta jasho kwa leso yake
chakavu. Akaliacha eneo hilo kwa mwendo wa asteaste huku akiwa na chupa ya maji
baridi mkononi na kijibegi chake begani.
Mfukoni alikuwa na
shilingi 250,000 tu ambazo alizichukulia kuwa ni kiasi kidogo cha pesa
kisichostahili kujivunia kutokana na majukumu mengi na muhimu yaliyokuwa mbele
yake. Lakini pamoja na hayo, bado aliamini kuwa akiwa makini katika matumizi,
fedha hizo zitatosha kwa jambo lolote alilodhamiria
kulifanya.
Alipanga kuanza operesheni yake kwa kuzungukia
magereza ya Keko, Ukonga na Segerea. Kama Shaka hatakuwa katika magereza hayo,
angeitumia siku hiyo kufanya utafiti zaidi, ajue gereza lililomhifadhi na
kumfuata hukohuko aliko hata kama ni mkoa mwingine.
Alianzia
Segerea. Jibu alilolipata huko ni kwamba hakukuwa na mfungwa mwenye jina la
Shaka, wala kwa wiki nzima iliyopita hawajawahi kumpokea mtu mwenye tuhuma nzito
kama alizowaeleza.
Akaenda
Ukonga.
Patupu!
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni katika gereza la
Keko ndipo alipopata jibu zuri. Askari mmoja alimwambia kuwa majuzi walimpokea
jambazi sugu mwenye jina hilo. Likawa ni jibu lililomtia faraja mzee Songoro.
Papohapo akatwaa mzizi ndani ya mfuko wa shati na kuutia mdomoni. Akaanza
kuutafuna taratibu bila ya kuumeza. Na alikuwa na sababu ya kufanya
hivyo.
Mzizi huo ulikuwa na nguvu za ajabu. Mtu yeyote akiutia
mdomoni, na kuutafuna huku akizungumza na mtu mwingine, basi chochote
atakachokisema huyo mtumiaji mzizi kitakubaliwa na
msikilizaji.
Watumiaji wengi wa mzizi huo ni wale wanaokwenda
mahali kutafuta ajira, wakware na wenye kesi mahakamani. Mzee Songoro alikuwa ni
miongoni mwa watu hao. Na alipoutia mzizi huo kinywani, matumaini ya mafanikio
yakazidi kumjaa.
Jumapili hiyo ilikuwa ni siku maalumu kwa
ndugu, jamaa na marafiki kuruhusiwa kuonana na wafungwa. Na nje ya gereza hilo
kulikuwa na umati mkubwa wa watu waliokuja kwa madhumuni hayo ya kuonana na
ndugu zao ambao baadhi walikuwa wakitumikia vifungo na baadhi walikuwa rumande
wakisubiri hukumu za kesi zilizowakaabili.
Mzee Songoro alikuwa
miongoni mwa watu hao. Akilini mwake aliamini kuwa kitendo cha kuruhusiwa
kuonana na Shaka kingetosha kuzaa matunda mema. Huo ungekuwa mwanzo
mzuri.
Hatimaye nafasi hiyo ikapatikana. Mzee Songoro akafurahi
kumwona mwanaye akiwa hai, mwenye afya njema japo alikuwa ndani ya mavazi ya
jela. Hata hivyo hakuanza kuongea naye bali alimfuata askari jela na kumwomba
kuzungumza na Shaka, faragha.
“Huo siyo utaratibu wetu, mzee,”
askari alimjibu. “Jaribu kufuata utaratibu kama wengine. Kwani kuna tatizo gani
hadi mkae pembeni?”
“Mwanangu,” Mzee Songoro alisema kwa sauti
ya upole, mzizi ukiendelea kutalii kinywani mwake. “Naomba utambue kuwa Shaka ni
mwanangu. Ni mwanangu wa kuzaa. Na mimi nimetoka mbali. Hebu fikiria, Kigoma
hadi hapa ni safari fupi? Tena usafiri wenyewe wa hii treni yetu isiyokuwa na
uhakika lini itasafiri na treni yenyewe iko hoi bin
taaban!”
Akatulia kidogo kisha akaendelea, “Uwe na utu
mwanangu. Nadhani na wewe una mtoto au watoto. Na kama huna, basi nadhani
utakuwanao. Damu nzito, mwanangu. Shaka ni damu yangu, sikumnunua
dukani.”
Ilitosha.
Sheria ya jela ikavunjwa!
Mzee Songoro akaruhusiwa kuketi faragha na mwanawe,
Shaka.
Hatua ya kwanza imefanikiwa!
Mzee
Songoro alikumbuka kuwa dakika tano alizopewa na yule askari jela ni chache
hivyo bila ya kupoteza muda alifungua mkoba wake na kutoa kichupa kidogo chenye
maji yaliyochanganywa na dawa ya unga maalumu. Kisha akatoa kijikaratasi kidogo
kilichokuwa na unga kidogo.
“Unaiona hii?” alimuuliza kwa
mnong’ono huku akimpa ile chupa ya maji. “Ifiche vizuri. Kesho asubuhi, yaani
ile alfajiri pwee, amka ujinyunyizie katika nguo zako. Matone mawili, matatu
yatatosha. Baada ya hapo unaweza hata kuitupa chupa hii. Umenielewa vizuri?”
alimkazia macho.
“Nakuelewa, baba.”
Sasa Mzee
Songoro akatoa kile kijikaratasi chenye unga na kumkabidhi Shaka. “Hii ni muhimu
sana,” alimwambia. “Elewa kuwa wewe nd’o mwan’etu wa pekee. Hatutaki kukupoteza!
Wewe nd’o taa ya maisha yetu! Umenisikia mwanangu?”
Shaka
aliitika kwa kutikisa kichwa huku akikitazama kile kijikaratasi chenye dawa ya
unga.
“Ficha vizuri dawa hii,” Mzee Songoro aliendelea. “Kesho
asubuhi ujipake usoni, mikononi na miguuni. Hakikisha unafanya hivyo bila ya mtu
mwingine kugundua. Dawa itakayosalia, tia kinywani na kuimeza.
Umenielewa?”
Kwa mara nyingine Shaka alitikisa kichwa
akiashiria kukubali. Hakushangazwa na maneno hayo ya baba yake. Aliyajua makali
aliyonayo katika nyanja ya ushirikina. Kwa kipindi hicho kifupi alijua kuwa
atakuwa na saa zisizozidi kumi na nane kabla ya utawala mzima wa gereza hilo
haujahaha kuhoji kuhusu yeye huku msako mkali dhidi yake ukiendeshwa ndani na
nje ya gereza hilo.
MZEE Songoro alimtazama yule
askari jela kwa chati. Akafurahi alipogundua kuwa alizamisha akili na macho yake
kwenye kundi lingine la watu waliokuwa wakiongea na ndugu zao ambao baadhi yao
kesi zao zilikuwa hazijaisha na baadhi wakiwa wamekwishaanza kutumikia
vifungo.
Kwa jinsi askari huyo alivyoonekana, Mzee Songoro
aliamini kuwa maongezi kati yake na Shaka hayakumfikia, hivyo kwa sauti ileile
ya mnong’ono aliendelea, “Ukishabugia dawa hii, subiri muda wa kwenda kwenye
kazi za nje.”
Akatulia na kuzidi kumkodolea macho Shaka. Kisha
akaongeza, “Wakati mtakapotolewa nje ndipo ujue kuwa ni muda wako wa kuwaacha.
Ukishajiona uko nje ya jengo hili tu, usizubae. Anza safari.”
Shaka aliguna.
Akashusha pumzi kwa nguvu. Kisha kwa sauti ya chini zaidi, akauliza, “Baba,
nitawezaje kufanya hivyo huku nikiwa na miguo hii ya
jela?”
“Usihofu,” Mzee Songoro alimtuliza. “Hutapata matatizo
yoyote! Utoke hivyohivyo ulivyo! Utakapokuwa mbali kidogo, ndipo utumie mbinu
zako upate nguo za kubadili. Una akili na una nguvu; sidhani kama utashindwa kwa
lolote.”
Wakatazamana huku wote wakiwa kimya. Kisha Mzee
Songoro akaendelea, “Ukishakuwa uraiani tafuta usafiri wa kukuleta Kigoma. Jiji
hili ni lako. Sidhani kama utashindwa kupata pa kujichimbia wakati ukitafuta
usafiri wa kukuleta nyumbani. Na huna haja ya kutumia usafiri wa hii treni yetu
isiyokuwa na uhakika wa kuondoka. Tumia usafiri wowote hadi ufike Kigoma ndani
ya siku mbili, tatu hivi zijazo.”
“Sina
pesa!”
“Hilo s’o tatizo,” Mzee Songoro alimtuliza. Papohapo
akaingiza mkono mfukoni na kuchomoa noti kumi za shilingi elfu kumi-kumi.
Akampatia Shaka kiuficho huku akinong’ona, “Laki hiyo.”
Shaka
naye akazipokea kisirisiri na kuzifutika kwenye mfuko wa kaptula
yake.
“Najua hizo pesa hazitoshi,” Mzee Songoro aliendelea.
“Lakini najua hutakwama. Nasema tena, nguvu unazo, akili unayo. Hakikisha kesho
hulali humu ndani. Utakapokuwa mitaani fanya unavyojua upate nyongeza ya pesa.
Lakini usiendelee kukaa hapa Dar. Uje nyumbani nikupe kinga kamili ya maisha
yako yote.”
Baada ya mzee Songoro kusema hayo, alimshika mkono
Shaka kwa nguvu huku akimtazama kwa macho makali, tabasamu la mbali likijiunda
katika uso wake uliosheheni mikunjo ya uzee. Kisha kwa mnong’ono mkali zaidi,
akasema, “Kwaheri mwanangu. Kwaheri. Tutaonana
nyumbani.”
Akatoka.
******
SAA
9 usiku, Shaka alizinduka usingizini. Akaangaza macho huku na kule. Akakunja pua
kutokana na harufu kali ya mchanganyiko wa jasho kutoka kwa wafungwa wengine
ambao walikuwa wakikoroma usingizini.
Akamtazama aliyekuwa
jirani yake upande wa kushoto. Huyo alikuwa hoi usingizini, ni kama alikuwa
ameyazoea maisha ya jela. Usingizi wake ulionekana kuwa ni wa kustarehe, kama
aliyelalia godoro zuri ndani ya chumba kizuri. Hata afya yake ilikuwa ikitoa
taswira kuwa ameridhishwa na mazingira aliyomo. Akamgeukia mfungwa wa upande wa
kulia. Huyo alikuwa kadhoofu na alikohoa mfululizo.
Hakuwajali.
Mawazo yake yalikuwa juu ya maagizo aliyopewa na baba yake.Taratibu akajitoa
pale sakafuni na kwa mwendo wa kunyata akaenda kusimama kiambazani, mkononi
akiwa na kile kijikaratasi chenye dawa ya unga na kijichupa kidogo chenye dawa
ya maji.
Hatua iliyofuata ilikuwa kufanya kile alichoelekezwa
na baba yake; kujinyunyizia matone matatu ya ile dawa ya majimaji nguoni kisha
akajipaka ule unga usoni, mikononi na miguuni kabla ya kuutia kinywani na
kuumeza.
Hakupaona mahali palipostahili kuitupa ile chupa,
hivyo aliirejesha mfukoni na kurudi kwenye malazi yake kwa mwendo uleule wa
kunyata.
Aliamini kuwa hakuna ambaye alimwona wakati
akiyatekeleza maagizo yale ya baba yake, na hata hivyo, pia alijipa imani kuwa
hata kama ameonwa na yeyote yule asiyehusika, bado hakutakuwa na
litakaloharibika.
Saa 11:30
alfajiri hakuna mfungwa aliyekuwa amelala. Pilikapilika za hapa na pale
zilitawala hadi anga ilipotakata. Muda wa kazi za nje ulipotimu, makundi kadhaa
yalipangwa. Shaka alikuwa katika kundi la wafungwa kumi ambao walitakiwa kwenda
kwenye ujenzi wa banda la maonyesho katika Viwanja wa Maonesho ya Biashara ya
Kimataifa vya Julius Nyerere.
Kundi hilo liliamriwa kupanda
ndani ya lori lililokuwa likiwasubiri. Askari jela alikuwa akifoka, akiwahimiza
kufanya haraka. Wafungwa, mmoja baada ya mwingine walianza kupanda garini.
Wakati huo, Shaka alikuwa nyuma akisitasita kuitii amri ya askari huyo. Mawazo
yake yalikuwa juu ya maagizo aliyopewa na baba yake mzazi, jana
yake.
Aliamini kuwa kama hatachukua uamuzi wa kuondoka hapo,
wakati huohuo, basi huenda akawa ametibua kila kitu kuhusu maagizo aliyopewa na
baba yake.
“Oyaa! We mtoa roho za watu, jambazi mkubwa unawaza
nini? Hii nd’o Keko! Usidhani uko kwa hawara yako huko uswazi! Panda gari
haraka!” Amri kutoka kwa askari jela iliyafikia masikio yake kwa
usahihi.
Ni amri hiyo iliyomzindua, na akazinduka. Papohapo
akaamua kuanza utekelezaji wa maagizo aliyopewa. Badala ya kuitii amri ile ya
askari, aligeuka na kuondoka. Akavuta hatua kwa mwendo wa taratibu lakini kwa
kujiamini, akiliacha eneo hilo.
Yule askari aliduwaa,
akamtazama bila ya kuchukua hatua yoyote. Shaka aliendelea kutembea taratibu,
bila ya kuonesha hofu yoyote. Alipotokeza barabarani akakutana na askari wengine
wawili wenye sare, ambao walimwangalia kidogo tu, kwa mshangao, kisha
wakaendelea na safari yao, yeye na safari yake.
Alipita hapa na
pale, kwa mwendo uleule wa kujiamini huku akiwa amekwishaitupa ile chupa
iliyokuwa na dawa ya unga kando ya barabara, mtaroni bila ya mtu yeyote mwingine
kubaini.
Hatimaye akaingia ndani ya duka moja ambako alimkuta
mwanamama akimhudumia mteja. Bado mwanamume Shaka hakuwa na wasiwasi. Alitulia
akisubiri mteja huyo aondoke, na baada ya dakika mbili, tatu akajikuta
akitazamana ana kwa ana na muuzaji yule.
“Karibu, kaka,”
muuzaji yule alimkaribisha huku akimtazama kwa mshangao.
Shaka
aliugundua mshangao wa muuzaji huyo, lakini hakujali. Alijua kuwa mavazi yake
ambayo ni sare rasmi ya mfungwa ndiyo yaliyomshangaza muuzaji
huyo.
Aliangaza macho pande zote za duka hilo. Lilikuwa ni duka
lililofurika bidhaa mbalimbali; vipodozi, vyakula vilivyosindikwa na
visivyosindikwa, soda hata bia na pombe kali. Pia, kulisheheni nguo za aina
mbalimbali za kike na kiume.
Alivutiwa na mashati pamoja na
suruali kadhaa zilizokuwa zimening’inizwa. Akalinyooshea kidole shati moja jeusi
la mikono mifupi lenye ua jekundu mgongoni. Akauliza, “Lile shati,
vipi?”
Muuzaji hakuchelewa, mara akalifuata na kulinyofoa,
kisha akampatia Shaka huku akisema, “Liangalie vizuri kaka’angu. Na kwa mwili
wako lazima litakupendeza.”
Shaka alilitwaa shati hilo,
akalitazama kidogo na kuliweka mezani. “Na ile suruali?” akainyooshea kidole
suruali nyeusi.
Kama alivyofanya kwa shati, muuzaji aliitoa
suruali hiyo na kumwachia huru Shaka aichunguze-chunguze.
Dakika ya pili Shaka
aliamua. “Nipe bei ya jumla,” alimwambia muuzaji huyo.
“Elfu
ishirini.”
“Chukua kumi na
tano.”
ITAENDELEA
0 Comments:
Post a Comment