Simulizi :
Mtikisiko Wa Hirizi
Sehemu Ya Tano (5)
“Huyo mtu kasemaje?”
Panga Sakanyoka alimdaka.
“Kwamba Mzee Songoro anaishi na mkewe na
mwanae mmoja tu, ambaye amekuja majuzi kutoka Dar. Anadai kuwa yeye anaishi
nyumba ya tatu kutoka kwa Mzee Songoro, na huwa anamwona Shaka kila asubuhi
akinawa uso nje ya nyumba hiyo.”
Banda na Panga Sakanyoka
walitazamana kisha Banda akasema, “Naona twende. Matokeo yote tutayapata
hukohuko. Kama yupo au hata hakulala hapo tutajulia
hukohuko.”
Maandalizi yakafanyika chapchap. Askari wengine kumi
wenye silaha wakawekwa tayari. Muda mfupi baadaye Land Rover ilikuwa barabarani
ikielekea Mtaa wa Mabatini.
Walipoikaribia nyumba hiyo waliteremka na
kuanza kupangiana majukumu.
Hawakutaka kuivamia nyumba hiyo
mapema kiasi hicho. Ilikuwa ndiyo kwanza inatimu saa 12.20. Bado kijigiza
kilitawala anga. Hivyo Panga Sakanyoka aliwapanga wale askari, akawapa majukumu
ya kuizingira ile nyumba na kuhakikisha kuwa hakuna mtu
atakayetoka.
“Lakini msifanye chochote,” Panga Sakanyoka
aliwaambia askari hao. “Kuweni makini, mkihakikisha hatoki mtu humo ndani, na
wala isije ikatokea kuwa jamaa yumo ndani na akagundua kuwa tumemzingira! Na
kuweni makini kwa huenda ana silaha. Kama ana silaha, akigundua kuwa amezingirwa
hataacha kuitumia. ”
**********
ILIKUWA ni
kawaida kwa Mzee Songoro kuzinduka usingizini saa 11 alfajiri. Na alfajiri hii,
kama alfajiri nyingine zilizopita pia alizinduka saa 11 lakini hakutoka
kitandani. Alibaki amekodoa macho huku akihisi hirizi iliyokuwa kiunoni mwake
ikicheza.
Kucheza kwa hirizi hiyo, kwake ilikuwa ni ishara kuwa
kuna tukio kubwa mbele yake. Na wazo lililomjia kichwani ni kumhusu mwanawe,
Shaka. Tangu Shaka arejee kutoka Dar, amekuwa mtu wa kutoka mara kwa mara, na
majuzi aligundua kuwa alikuwa na pesa nyingi.
Mzee Songoro
hakupenda kujidanganya kuwa Shaka anaweza kuwa amezipata pesa hizo kwa njia
yoyote ya halali. Alijua kuwa kuna mtu au watu ‘waliolizwa.’ Kitendo cha hirizi
hii kucheza kilimpa ishara kuwa Polisi walikuwa wameshamshuku Shaka kuwa ni
mhusika wa matukio mawili makubwa ya majuzi; kuuawa kwa wale wakazi wawili wa
Lumumba Road na Kibirizi Road.
Hata hivyo, kwa kuwa alijiamini,
hakuwa na wasiwasi. Alijua jinsi ya kutatua tatizo lolote litakalotokea.
Akanyanyuka kitandani na kutwaa msokoto wa tumbaku uliokuwa umehifadhiwa vizuri
kwenye kipande cha gazeti. Akauwasha na kuanza kuvuta taratibu. Akamtazama mkewe
ambaye bado alikuwa ametopea usingizini. Akamwacha. Hakuwa na sababu ya
kumzindua na kumshirikisha katika hisia zake za hirizi kutikisika
kiunoni.
Saa 12 alfajiri ilimkuta papohapo kitandani aking’aa
macho. Mara akasikia kikohozi kizito kutoka chumba cha pili. Hakikuwa kikohozi
kigeni masikioni mwake. Alishakizoea. Ni kikohozi kilichomtambulisha kuwa
mwanaye, Shaka yumo chumbani mwake.
Hirizi kiunoni mwake
ilizidi kutikisika.
Mara akasikia vishindo vya miguu nje ya
nyumba, vishindo vizito vya watu waliokuwa wakitembea taratibu. Hirizi ikazidi
kutikisika. Sasa akauzima msokoto wake wa tumbaku.
Akajitoa kitandani na
kwenda sebuleni huku kavaa msuli peke yake. Akasimama katikati ya sebule huku
akiuangalia mlango wa chumba cha Shaka.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hirizi ikazidi
kutikisika kiunoni! Na sasa ikawa kama inayomtekenya.
Mara
mlango ukagongwa. Mzee Songoro akashtuka na kuutupia macho. Ukagongwa tena,
safari hii kwa nguvu zaidi. Mzee Songoro akahisi hatari. Haukuwa ugongaji wa
heri. Hata hivyo akapiga moyo konde na
kuufuata.
Akaufungua.
MACHO yake yakakutana na
ugeni wa ajabu. Moyo ukapiga paa! Kupatwa na mshtuko mkubwa pindi aonapo au
asikiapo chochote huwa ni ishara mbaya kwake. Na jambo lingine ambalo huashiria
hali mbaya huwa ni pale hirizi aliyovaa kiunoni inapoanza kumbughudhi kwa
kujitikisatikisa.
Ni bibi yake ambaye alimpa tahadhari kuhusu ishara
hizo kabla hajafariki. Na ni bibi yake huyohuyo aliyempika, akaiva na kutokota
vilivyo katika nyanja ya ushirikina.
Mara kwa mara alikuwa
akienda kwenye makaburi ya Katubuka ambako marehemu bibi yake alizikwa zaidi ya
miaka thelathini iliyopita. Alikuwa akienda huko kufanya tambiko maalumu kama
ilivyo kawaida katika mila na desturi za kabila lao la Kibembe. Na kwa kufanya
hivyo aliamini kuwa ndipo mambo yake yangeendelea
kunyooka.
Sasa akaamua kuwa makini. Mbele yake walisimama
wanaume watatu waliovaa kinadhifu. Akawatazama kwa makini nyusoni na kugundua
jambo moja. Sura zao zilitangaza kazi zao.
“Askari!”
alinong’ona kwa sauti ambayo haikuweza kuyafikia hata masikio yake mwenyewe.
Hata hivyo alijiamini, na kwa sauti ya kujiamini vilevile alisema,
“Karibuni…karibuni vijana.”
Ni Inspekta Banda aliyetangulia
kuingia akifuatiwa na Sajini Kessy kisha afande Panga Sakanyoka. Wakamsalimia
kwa heshima huku wakionyesha nyuso za bashasha. Na Mzee Songoro akiwa na umakini
wa hali ya juu, hakudanganyika kwa nyuso hizo za tabasamu bali naye
aliwakaribisha kwa mfumo huohuo.
“Mzee tumetoka kituo cha
Polisi,” Inspekta Banda alianza kuzungumza, sasa sura yake ikiwa imeshabadilika,
tabasamu likiwa limeshayeyuka. “Tunataka utupe taarifa kuhusu mwanao,
Shaka.”
“Shaka?” Mzee Songoro alijitia kushangazwa na swali
hilo.
“Ndiyo, Shaka,” Banda alisisitiza. “Yupo? Kama yupo
mwambie atoke na ajisalimishe. Hatutaki kutumia nguvu. Tumekuja kistaarabu,
tuondoke kistaarabu.”
Mzee Songoro aliguna. “Vijana, mbona
siwaelewi?” hatimaye aliwauliza.
“Kitu gani ambacho hukielewi?”
Panga Sakanyoka alimbana. “Umeambiwa kamtoe Shaka huko ndani, eti unadai kuwa
hutuelewi. Una maana gani mzee?”
Tabasamu la kujiamini lilizidi
kuchanua usoni pa Mzee Songoro. Akawatazama kwa zamu askari hao. Kisha akasema,
“Mnanishangaza kwa kauli yenu, vijana. Shaka ni mwanangu, ndiyo. Lakini nina
mwaka sasa sijamtia machoni. Aliondoka hapa akaelekea Dar, na majuzi tu
nimesikia taarifa kuwa amekamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha hukohuko
Dar!”
“Umeisikia wapi taarifa hiyo?” Banda alimdaka kwa
swali.
“Nilikuwa nikiangalia taarifa ya habari kwenye
televisheni, nd’o nikaipata taarifa hiyo.”
“Una hakika kuwa
Shaka aliyetangazwa kwenye televisheni ndiye huyo
mwanao?”
“Jina. Lilitajwa jina la Shaka
Songoro.”
“Yaani mwenye jina la Shaka hapa duniani ni mmoja tu,
huyo mwanao, na mwenye jina la Songoro pia ni mmoja tu, wewe. Si nd’o
maana’ake?” Panga Sakanyoka
alimuuliza.
“Hapana.”
“Sasa
kumbe?”
“Pamoja na habari ile kutangazwa, hata picha yake
ilionyeshwa.”
“Taarifa hiyo ilisema kuwa amehukumiwa kifungo?”
Kessy alimdaka.
“Ndiyo.”
“Kwa kosa
gani?”
Akilini mwa Mzee Songoro aliliona swali hilo kuwa la
kimtego. Lakini ulikuwa ni mtego alioweza kuutegua. “Hata mimi sijui lilikuwa ni
kosa gani,” hatimaye alijibu. Akaongeza, “Hata habari yenyewe niliisikia ikiwa
ni muhtasari wa mwisho.”
“Hata hivyo tunajua kuwa Shaka yuko
hapa!” Panga Sakanyoka alisema kwa ukali. “Sema ukweli wako kabla hatujaamua
kuchukua hatua nyingine. Yupo au hayupo?”
“Hayupo!” Mzee
Songoro alijibu kwa msisitizo.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mzee,” Inspekta Banda
alimnyooshea kidole. “Usidhani kuwa tunakuogopa. Usijidanganye kwa hilo.
Tukitaka, tunaweza kuondoka na wewe na kwenda kukusweka ndani sasa hivi!
Hatuujali umri wako, utatupwa ndani, na kibano utakachokipata huko kitakufanya
uutapike ukweli, kama kwa sasa umeshindwa kuusema.
Umeelewa?”
Mzee Songoro alicheka kidogo. “Vijana mna vituko!
Yaani mnataka kuniweka ndani kwa kosa lisilo langu!”
“Utatupwa
ndani kwa kosa lako!” Panga Sakanyoka alijibu.
“Kosa
gani?”
“Hilo sio
swali.”
*********
SHAKA alikuwa
kitandani kajilaza huku akisikiliza maongezi kati ya baba yake na wageni
walioingia. Alijua kuwa wageni hao ni askari, na wamekuja kumkamata. Akavuta
pumzi ndefu na kunyanyuka. Akasimama na kulifuata begi lake, akalifungua,
akautoa msokoto wa bangi na kuuweka juu ya meza.
Hakuishia
hapo, aliichukua pakiti ya sigara na kuchomoa sigara moja. Akaichokonoa na
kupunguza tumbaku iliyomo kisha akachomeka bangi. Ukawa ni mchanganyiko maalumu
aliouhitaji.
Kilichofuata, aliuwasha mchanganyiko huo wa sigara
na ile bangi kisha akavuta mikupuo miwili ya nguvu. Akili ikachangamka! Papohapo
akazivamia nguo zake na kuzivaa. Akaitwaa bastola na kuifungua haraka katika
kuchunguza idadi ya risasi zilizomo.
Akaridhika baada ya kukuta
kuna risasi sita. Akaifunga huku akiachia tabasamu hafifu, tabasamu
lililofuatiwa na kicheko cha chini sana lakini cha kujiamini. Kila anapokuwa
anamiliki chombo cha aina hiyo, chenye gololi kadhaa ndani yake, basi hujiona
kuwa yuko salama, hakuna chochote kitakachomletea taabu.
Katika
muda huo, alitambua kuwa alipaswa kufanya chochote kile ili anusurike. Aliamini
kuwa hatima ya maongezi au mabishano kati ya baba yake na hao askari, ni askari
kuvivamia vyumba vyote vya nyumba hiyo kwa upekuzi. Na alijua kuwa matokeo ya
upekuzi huo ni yeye kujikuta katika wakati mgumu zaidi.
Akaamua
kuchukua uamuzi wa haraka, lakini ukiwa ni uamuzi alioamini kuwa ungemnufaisha
kwa asilimia mia moja.
Papo hapo akatupa macho dirishani na kujiwa na
wazo la kupitia hapo ili atoke chumbani humo. Hiyo ikiwa ni nyumba ya kawaida,
iliyojengwa kwa mianzi na kukandikwa udongo wa mfinyanzi, haikuwa na ukuta
ulioweza kuhimili konde moja zito la kono la kulia la
Shaka.
Hivyo, hata hilo dirisha halikuwa katika hifadhi
madhubuti kiasi cha kuweza kuwa kikwazo kwake. Kwa kutumia nguvu alizojaaliwa,
alilishika dirisha hilo na kulitikisa mara mbili; nje, ndani, nje, ndani! Jibu
likapatikana.
Dirisha liling’oka!
Mwanamume
akachupa nje! Huko alitua kwa kishindo kikubwa puu! Wakati akichukua uamuzi huo
hakuwa na wazo kuwa huenda ulinzi katika eneo hilo umeimarishwa hadi nje ya
nyumba. Hivyo hakumwona askari aliyekuwa kando ya dirisha hilo, ambaye alikuwa
tayari kwa utekelezaji baada ya kuusikia kukurukakara za kung’olewa kwa dirisha
hilo.
Wakati Shaka alipoanza kuigeuza shingo yake kutazama
upande wa kulia, askari yule hakumpa nafasi. Alimwahi kwa konde zito la shavuni,
konde ambalo kwa Shaka lilikuwa limemkuna tu na kumtambulisha kuwa amekumbana na
adui.
Akili yake ikafanya kazi maradufu. Alikuwa mwepesi na
alikuwa na nguvu, hivyo alimtazama askari huyo kwa sekunde moja tu, sekunde ya
pili alikuwa amemsukumia konde kwa kono la kushoto, konde lililotua sawia
kidevuni mwa askari huyo na kumpeleka chini, taya likiwa halina
kazi!
Shaka akahema kwa nguvu huku akitupa macho huku na kule.
Kwa jumla alijiona bado yuko katika kipindi kigumu zaidi. Alitarajia kuwa kuruka
dirishani ingekuwa ni hatua ya kwanza katika kujiweka kwenye mazingira mazuri ya
kutokumbwa na mshikemshike wa askari hao. Lakini kumbe hajafanya lolote!
Amekumbana na askari huku nje, na askari huyo akiwa ana silaha. Hilo tu
lilitosha kumfanya ajue kuwa kuna askari mwingine au wengine zaidi ya wale
waliokuwa ndani wakimsumbua baba yake.
Kwa hali hiyo aliamini
kuwa bastola peke yake isingetosha kukabiliana na misukosuko iliyokuwa mbele
yake. Ndipo alipoinama na kuitwaa bunduki iliyokuwa kando ya yule askari
aliyekuwa hoi akikoroma. Akaikamata madhubuti mikononi na kuanza kuufuata
uchochoro uliokuwa mbele yake huku akiwa makini katika
kujilinda.
Alikuwa hajavuta hata hatua kumi mara risasi
zikamiminika katika uelekeo wake. Akashtuka! Sasa badala ya kutembea, akakimbia
hadi kwenye kiambaza cha nyumba ya pili ambako alibana na kuikamata bunduki
vizuri tayari kwa kukabiliana na lolote.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sekunde kadhaa zikapita
kukiwa na utulivu, kisha akawaona askari takriban kumi wakiwa na bunduki
mikononi.
Askari hao walionyesha kuwa wanamtafuta. Ni hapo ndipo
kumbukumbu ya kinga aliyofanyiwa na baba yake ilipomjia kichwani!
Hirizi!
Wahaka ukamtoka, ujasiri ukamjaa! Akainua bunduki na
kufyatua risasi kadhaa mfululizo. Askari watano, mmoja baada ya mwingine
walianguka chini, maiti! Hakutulia, aliendelea kuitumia bunduki hiyo kikamilifu.
Kipindi kingine kifupi kilichofuatia askari wengine wanne walifuata nyayo za
wenzao.
Naam, ulikuwa ni kama muujiza! Askari waliendelea kupukutika
huku Shaka akiwa hana hata
jeraha!
*********
KULE ndani Inspekta Banda
aliwatazama wenzake kwa mshangao, bastola ikiwa mkononi. Mkuu wa Kitengo cha
Upelelezi, Panga Sakanyoka alikuwa amechanganyikiwa wakati Sajini Kessy
alionekana kama anayejaribu kukumbuka jambo fulani.
Ukimya
ukatawala kwa muda mfupi. Kisha, kama aliyezinduliwa usingizini Sajini Kessy
alisimama, bastola ikiwa mkono wa kulia, akawatazama Banda na Panga Sakanyoka
kwa zamu, na kwa sauti ya kujiamini akasema, “Nakwenda…! N’achieni n’ende..
n’takufa naye!”
Hakusubiri ruhusa, alitoka kasi hadi nje ambako
alimwona Shaka umbali wa hatua kama ishirini na huku maiti za askari zikiwa
zimetapakaa huku na kule. Wakagonganisha macho, dalili za kuua zikiwa bayana
ndani ya mboni za macho yao!
Shaka alikuwa na bunduki na Kessy alikuwa
na bastola! Kila mmoja alikuwa mwepesi wa kuuinua mkono na kumwelekezea mwingine
silaha, hivyo kila mmoja kujikuta akitazamana na kifo!
Hata
hivyo, ni Shaka aliyekuwa mwepesi wa kufikiri na kutekeleza kwa haraka uamuzi
wake. Alifyatua haraka risasi moja bila ya shabaha kamili. Risasi hiyo ikamkosa
Kessy kidogo sana.
Lilikuwa ni jambo lililomfanya Sajini Kessy
ahisi kuwa kifo kilikuwa kikimnyemelea kwa kasi ya kutisha. Hivyo akaamua
kuchukua hadhari kubwa zaidi. Akajirusha hadi ndani ya banda
moja.
Ujenzi wa banda hilo ulikuwa haujakamilika, hata hivyo
urefu wa ukuta wake ulitosha kumhifadhi mtu yeyote aliyeinama au kuchuchumaa.
Kessy aliporukia ndani alichuchumaa na kujiandaa kukabiliana na mashambulizi ya
Shaka. Moyoni mwake alijua kuwa kazi iliyomkabili mbele yake ni kubwa kuliko
alivyofikiria na kukadiria. Adui yake alikuwa na silaha nzito, iwezayo kumwaga
risasi kama mvua. Yeye alikuwa na bastola yenye risasi tatu! Hivyo,
timbwili-timbwili lililokuwa mbele yake aliamini kuwa halitakuwa la
kawaida.
Kazi nzito, alijisemea kimoyomoyo huku akikumbuka
jinsi alivyowaaga wenzake, maafande wake kule ndani kuwa anajitoa mhanga kumvaa
Shaka, na kwamba yuko tayari kwa lolote. Ni kauli ile aliyoitoa kule ndani na
kutoka bila ya kusubiri ruhusa yao, ndiyo iliyomfanya ajipe ujasiri wa aina yake
na kuamua kuitimiza nadhiri aliyokwishaiweka. Aliamua kufa au
kupona!
Anga ilikuwa ikizidi kutakata. Jua lilichomoza
mashariki na kushusha miali yake ardhini, hali iliyomfanya Kessy ajawe na
matumaini ya kufanikisha lolote lile alilodhamiria kulitekeleza. Katika
kukamilisha azma yake ya kumpata Shaka akiwa hai au maiti, mwangaza wa jua
ulikuwa ni muhimu sana kwake.
Aliamini kuwa, mwangaza huo wa jua ndiyo
utakaotoa ufumbuzi wa kizungumkuti hicho. Lakini pia aliamini kuwa alipaswa kuwa
makini na kuchukua hadhari kubwa dhidi ya Shaka, mtu ambaye hakutofautiana na
shetani.
Dakika mbili, tatu zilikatika wanaume hao wakiwindana.
Mara kadhaa walirushiana risasi ambazo hazikuzaa matunda kwa upande
wowote.
Hatimaye ikatimu dakika ambayo huenda Kessy aliihitaji
kuliko dakika nyingine zote zilizotangulia! Shaka alikuwa ‘peupe’ akimulikwa
vizuri na miali ya jua. Kessy aliikamata bastola yake vizuri na kuielekeza
kwenye kivuli cha Shaka kisha akafyatua risasi moja iliyosalia katika bastola
yake.
Kilichotokea kilikuwa hakitofautiani na muujiza! Kessy
alifyatua risasi akikilenga kivuli cha Shaka badala ya kumlenga
mlengwa!
Shaka alitoa yowe kubwa, akaruka juu kidogo kisha
akaanguka chini, tii! Chali, bunduki ikiwa imemtoka mkononi na kuanguka hatua
chache kulia kwake!
Hakuvuta pumzi zaidi ya sekunde
tano!
**********
LILIKUWA ni tukio lililozua
patashika vichwani mwa Inspekta Banda na Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi, Panga
Sakanyoka. Hawakuamini mara moja kuwa Sajini Kessy amefanikiwa kumuua jambazi
hatari, Shaka Songoro kwa namna ya ajabu kiasi kile.
Wangeamini
vipi wakati tangu enzi na enzi kifo hutokea pale tu risasi inapozama mwilini
moja kwa moja na wala siyo kwa kupitia katika kivuli cha mlengwa? Na kuna
uhusiano gani kati ya kivuli na umbo halisi? Mbona hata hao wazungu
waliozitengeneza silaha hizi hawajaivumbua teknolojia hiyo ya ajabu?CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kulikuwa na
giza nene mbele ya askari hao. Na
hata wakati maiti ya Shaka
ilipofikishwa katika Hospitali Kuu ya Mkoa, Maweni, wao waliharakisha kukutana
ofisini ambako waliamua kumdadisi Sajini Kessy.
“Hili ni jambo
la kushangaza, Sajini,” Panga Sakanyoka alisema huku akimtazama Sajini Kessy kwa
macho makali. “Naamini hata RPC akisikia habari hizi, japo atafurahi lakini pia
atashangaa sana.
“Mauaji aliyoyafanya yule mshenzi yalikaribia
kumtia wazimu mzee wa watu, na siyo yeye peke yake. Hata sisi wengine tulikuwa
tumebaki njiapanda, zaidi ni kama vile tulikuwa tukitapatapa. Nadhani RPC
alikwishaamini kuwa Shaka ni shetani la aina ya kipekee, hivyo, kukamatwa au
kuuawa ni jambo lisilowezekana. Ndiyo maana kabla hamjaitwa, hakuwa na imani na
sisi -askari wa hapa.”
“Lakini sasa ataamini,” Inspekta Banda
alisema huku tabasamu la mbali likichanua usoni pake.
“Ndiyo
ataamini lakini atahoji sana ni mbinu gani tuliyotumia hadi kummaliza mshenzi
huyo,” Panga Sakanyoka alisema.
“Kuzijua mbinu tulizotumia kutamsaidia
nini?” Kessy alihoji huku naye akitabasamu.
Panga Sakanyoka
alikohoa kidogo. Yeye, tofauti na wenzake, kwa muda wote huo uso wake haukuwa na
tabasamu hata la bandia. Alionyesha wazi kusumbuliwa na jambo kichwani
mwake.
Akasema, “Yule nd’o bosi wa mkoa. Ni msemaji mkuu kwa
masuala yote ya kipolisi hapa Kigoma. Kwa vyovyote lazima ataniuliza mimi, na
mimi sijui chochote.” Papohapo akamkazia macho Sajini Kessy na kuongeza, “Wewe
nd’o unaweza kutufumbulia kitendawili hiki.”
Tabasamu la Sajini
Kessy liliendelea kuchanua usoni, kisha kwa sauti ya kujiamini alisema, “
Ilikuwa ni kazi ndogo tu, afande. Nakumbuka jana asubuhi wakati wa kikao na RPC
niliahidi kumtia mikononi Shaka. Kumkamata au kumuua! Sikuwa nabahatisha, wala
sikuwa natoa hadithi ya kubuni. Nilikuwa na hakika ya
n’nachokisema!”
Alishusha pumzi ndefu, akameza funda la mate
kisha akaendelea, “Afande, majambazi wengi wa huku Kigoma wana tabia ya
kuushirikisha ushirikina katika kazi zao. Naifahamu vizuri Kigoma hii;
nimezaliwa hapa, nimekulia hapa na nimesomea hapa. Kwa nini nisiyajue vizuri
mazingira ya hapa?
“Namfahamu vizuri Mzee Songoro,” aliendelea.
“ Habari zake nimeanza kuzisikia tangu utotoni. Anasifika kwa mambo ya
ushirikina. Ni mchawi wa kipekee! Na katika mizunguko yangu ya jana nimedokezwa
kuwa yeye ndiye nguzo kuu ya Shaka.”
“Yaani anamkinga
kiuchawi?” Inspekta Banda aliuliza.
“Nd’o
maana’ake.”
“Hilo ni jambo linalowezekana?” Panga Sakanyoka
alihoji kwa namna ya kutomwamini Kessy.
“Ni jambo
linalowezekana, afande,” Sajini Kessy alijibu kwa mkazo. “Japo si vizuri kwa
kofia zetu za dola kujenga imani za kishirikina, lakini huo nd’o ukweli wenyewe.
Mzee huyo alimpa kinga mwanaye ili asidhurike. Ndiye kinara wa mpango wote wa
Shaka tangu alipotoroka kule gerezani. Lakini…”
Alisita kidogo
na kumeza tena funda la mate, kisha akaendelea, “Hata hivyo namshukuru sana
marehemu, baba’angu mzazi.”
“Kwa nini?” Panga Sakanyoka
alimuuliza huku akimtumbulia macho.
“Ni yeye aliyenidokeza juu
ya mbinu ya kummaliza mtu ambaye hafi kwa mkuki, mshale, kisu, panga au
risasi.”
“Ni hiyo tunayohitaji kuijua!” Panga Sakanyoka
alionyesha shauku ya kuteguliwa kitendawili hicho.
Sajini Kessy
alimtazama Inspekta Banda kisha akayahamishia macho kwa Panga Sakanyoka,
tabasamu lake likizidi kuchanua. Na akionekana kutokuwa na haraka, akasema,
“Mzee Songoro anaweza kutufumbulia kitendawili hiki. Ni vyema tumtoe mahabusu
aje kutupatia hadithi kamili.”
Muda mfupi baadaye Mzee Songoro
alikuwa ameketi sakafuni, mbele ya askari hao. Machoni mwake, hakuonekana kuwa
na wasiwasi wowote. Aliwatazama askari hao kwa zamu, kisha akacheka kwa sauti
yenye mkwaruzo, kitendo kilichowashangaza askari hao.
“Unacheka
nini we’ mzee?” Banda alimuuliza huku akimtazama kwa macho
makali.
“Unataka ninune?” badala ya kujibu, Mzee Songoro naye
alimuuliza, sauti yake ikiwa ni ya kujiamini, akimtazama bila hata ya chembe ya
woga.
Akaendelea, “ Sina sababu ya kununa, nina sababu ya
kusikitika. Na siyo lazima nisikitike kwa kuwaonyesha usoni kuwa nimesikitika.
Japo mmemuua mwanangu kipenzi, hata hivyo sina budi kumpongeza sana kijana
huyu,” akamnyooshea kidole Sajini Kessy.
CHANZO :
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Banda na Panga
Sakanyoka wakayahamishia macho kwa Kessy. Wakamtazama kwa nukta chache tu na
kumrudia Mzee Songoro.
“Ni kijana hatari sana na shupavu
vilevile!” Mzee Songoro aliendelea. “Sikudhani kuwa kuna yeyote ambaye angeweza
kuigundua siri ya nguvu na uwezo wa kinga ya hirizi iliyo kiunoni mwa marehemu
mwanangu. Kwa kweli kijana huyu amefanya jambo la ajabu
sana…”
“Siki’za mzee,” Panga Sakanyoka alimkata kauli.
“Hatutaki mahubiri. Toa siri iliyofanya mwanao asipatwe na risasi! Hatutaki
mlolongo wa maneno kama unatusimulia riwaya hapa!”
“Huko ndiko
tunakoelekea, bwa’mdogo,” Mzee Songoro alisema bila hata ya chembe ya woga.
Akajipapasa katika boksa yake iliyokuwa ndani ya kanzu ndefu aliyovaa. Mara
akautumbukiza mkono katika mfuko mmoja wa boksa hiyo na kuutoa ukiwa na kibiriti
na msokoto wa tumbaku. Akauwasha msokoto ule na kuvuta mikupuo miwili, mitatu ya
nguvu kisha akauzima.
Moshi mzito, wenye harufu kali ukatapakaa
ofisini humo. Moshi huo ulikuwa ni kero tupu kwa askari wengine, siyo Inspekta
Banda ambaye alikuwa mvutaji wa sigara na zaidi, enzi za kukua kwake aliwahi
hata kuvuta bangi na tumbaku za kusokota.
Hata hivyo, kero hiyo
haikuwa ya kudumu kwa askari hao. Walivumilia kwa dakika moja hivi na hali
ikarudi kuwa ya kawaida.
“Shaka alikuwa ni mwanangu wa pekee,”
hatimaye aliendelea. “Nilimpenda sana. Kwa hivyo niliamua kumlinda; nikamfanyia
zindiko la pekee, zindiko kubwa. Katika zindiko hilo, nilimpatia hirizi ambayo
ilimfanya asidhurike; si kwa risasi tu bali hata kwa panga, kisu, mshale, mkuki
hata nondo. Ili uweze kumdhuru ulipaswa kushughulika na kivuli chake
tu!”
“Kivuli?” Inspekta Banda na Panga Sakanyoka walibwata kwa
pamoja.
“Ndiyo, kivuli chake tu!” Mzee Songoro alisisitiza. “Na
ndivyo alivyofanya huyu kijana wenu. Eti bwa’mdogo?” kufikia hapo alimgeukia
Sajini Kessy.
“Ndiyo,” Kessy alijibu huku akiachia tabasamu
dhaifu.
“Uliipata wapi mbinu hiyo?” Mzee Songoro
alimuuliza.
Kessy hakujibu. Badala yake alilizidisha tabasamu
lake huku akiwatupia macho kwa zamu Banda, Panga Sakanyoka na Mzee
Songoro.
“Najua hutaki kuitoa siri hiyo,” Mzee Songoro alisema
huku akikenua meno na kuupeleka tena ule msokoto wa tumbaku yake mdomoni.
Akavuta mkupuo mmoja na kutulia. Muda mfupi baadaye moshi ukatoka kwa kupitia
mdomoni na puani.
Akakohoa kidogo na kuutupa msokoto ule
sakafuni kisha akausaga na kandambili zake chakavu. Akamkodolea macho Inspekta
Banda na kwa sauti ya unyonge akasema, “Mwanangu amekufa. Mmemuua mwanangu wa
pekee. Sikutarajia kama ingetokea hivi! Wallahi sikutarajia! Mwanangu kafa
kiajabuajabu!”
Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi mkoani Kigoma,
Panga Sakanyoka, alishusha pumzi ndefu, akamtazama Mzee Songoro kwa macho makali
yasiyopepesa. Alipowageukia wenzake akamwona Inspekta Banda akimtazama Sajini
Kessy kwa namna ya kumpongeza. Wote wakatabasamu.
Hata wakati
Mzee Songoro aliponyanyuka na kuondoka mbele yao, wao walikuwa wameduwaa,
wakitazamana, huku wakitabasamu.
Ni Inspekta Banda
aliyewazindua akisema, “Hakuna cha kutukalisha hapa. Huyu mzee hakuna haja ya
kuhangaika naye. Kilichobaki ni RPC kuwaita waandishi na kulitangazia taifa kuwa
kikosikazi kimemaliza
kazi!”
MWISHO
Yes broo Appreciate
ReplyDelete